Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 10:22-42

Yohana 10:22-42 NEN

Wakati huo ilikuwa Sikukuu ya Kuwekwa wakfu kwa Hekalu huko Yerusalemu, nao ulikuwa wakati wa majira ya baridi. Naye Yesu alikuwa akitembea ndani ya Hekalu katika ukumbi wa Solomoni. Wayahudi wakamkusanyikia wakamuuliza, “Utatuweka katika hali ya mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo tuambie waziwazi.” Yesu akawajibu, “Nimewaambia, lakini hamwamini. Mambo ninayoyatenda kwa jina la Baba yangu yananishuhudia. Lakini hamwamini, kwa sababu ninyi si wa kundi la kondoo wangu. Kondoo wangu huisikia sauti yangu nami nawajua, nao hunifuata, nami ninawapa uzima wa milele, hawataangamia kamwe wala hakuna mtu atakayewapokonya kutoka mikono yangu. Baba yangu aliyenipa hawa ni mkuu kuliko wote na hakuna awezaye kuwapokonya kutoka mikononi mwake. Mimi na Baba yangu tu umoja.” Kwa mara nyingine Wayahudi wakainua mawe ili wampige nayo, lakini Yesu akawaambia, “Nimewaonyesha miujiza mingi mikubwa kutoka kwa Baba yangu. Ni ipi katika hiyo mnataka kunipiga mawe?” Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa sababu ya mambo mema uliyotenda, bali ni kwa kuwa umekufuru. Wewe ingawa ni mwanadamu unajifanya kuwa Mungu.” Yesu akawajibu, “Je, haikuandikwa katika Sheria ya kwamba, ‘Nimesema kuwa, ninyi ni miungu?’ Kama aliwaita ‘miungu,’ wale ambao neno la Mungu liliwafikia, nayo Maandiko hayawezi kutanguka, je, mwawezaje kusema kwamba yule ambaye Baba amemweka wakfu na kumtuma ulimwenguni anakufuru, kwa sababu nilisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu?’ Ikiwa sifanyi kazi za Baba yangu, basi msiniamini, lakini ikiwa nazifanya kazi za Mungu, hata kama hamniamini mimi ziaminini hizo kazi, ili mpate kujua na kuelewa kwamba Baba yu ndani yangu, nami ndani yake.” Ndipo wakajaribu kumkamata kwa mara nyingine, lakini akaponyoka kutoka mikononi mwao. Akaenda tena ngʼambo ya Mto Yordani mpaka mahali pale ambapo Yohana alikuwa akibatiza hapo awali, naye akakaa huko. Watu wengi wakamjia, nao wakawa wakisema, “Yohana hakufanya muujiza wowote, lakini kila jambo alilosema kumhusu huyu mtu ni kweli.” Nao wengi wakamwamini Yesu huko.