Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yn 10:22-42

Yn 10:22-42 SUV

Basi huko Yerusalemu ilikuwa Sikukuu ya Kutabaruku; ni wakati wa baridi. Naye Yesu alikuwa akitembea hekaluni, katika ukumbi wa Sulemani. Basi Wayahudi walimzunguka, wakamwambia, Hata lini utatuhangaisha nafsi zetu? Kama wewe ndiwe Kristo, utuambie waziwazi. Yesu akawajibu, Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia. Lakini ninyi hamsadiki, kwa sababu hammo miongoni mwa kondoo wangu. Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. Mimi na Baba tu umoja. Basi Wayahudi wakaokota mawe tena ili wampige. Yesu akawajibu, Kazi njema nyingi nimewaonyesha, zitokazo kwa Baba; kwa ajili ya kazi ipi katika hizo mnanipiga kwa mawe? Wayahudi wakamjibu, Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu. Yesu akawajibu, Je! Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu? Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu; (na maandiko hayawezi kutanguka); je! Yeye ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni, ninyi mnamwambia, Unakufuru; kwa sababu nalisema, Mimi ni Mwana wa Mungu? Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba. Wakatafuta tena kumkamata; lakini akatoka mikononi mwao. Akaenda zake tena ng’ambo ya Yordani, mpaka mahali pale alipokuwapo Yohana akibatiza hapo kwanza, akakaa huko. Na watu wengi wakamwendea, wakasema, Yohana kweli hakufanya ishara yo yote, lakini yote aliyoyasema Yohana katika habari zake huyu yalikuwa kweli. Nao wengi wakamwamini huko.