Yohana 13:18-30
Yohana 13:18-30 NENO
“Sisemi hivi kuhusu ninyi nyote. Ninawajua wale niliowachagua. Lakini ni kutimiza andiko lisemalo, ‘Yeye aliyekula chakula changu ameinua kisigino chake dhidi yangu.’ “Ninawaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa Mimi ndiye. Amin, amin nawaambia, yeyote anayempokea yule niliyemtuma anipokea mimi, naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenituma mimi.” Baada ya kusema haya, Isa alifadhaika sana moyoni, akasema, “Amin, amin nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.” Wanafunzi wake wakatazamana bila kujua kuwa alikuwa anamsema nani. Mmoja wa wanafunzi wake, ambaye Isa alimpenda sana, alikuwa ameegama kifuani mwa Isa. Simoni Petro akampungia mkono yule mwanafunzi, akamwambia, “Muulize anamaanisha nani.” Yule mwanafunzi akamwegemea Isa, akamuuliza, “Bwana, tuambie, ni nani?” Isa akajibu, “Ni yule nitakayempa hiki kipande cha mkate baada ya kukichovya kwenye bakuli.” Hivyo baada ya kukichovya kile kipande cha mkate, akampa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni. Mara tu baada ya kukipokea kile kipande cha mkate, Shetani akamwingia. Isa akamwambia Yuda, “Lile unalotaka kulitenda, litende haraka.” Hakuna hata mmoja wa wale waliokuwa wameketi naye mezani aliyeelewa kwa nini Isa alimwambia hivyo. Kwa kuwa Yuda alikuwa mtunza fedha, wengine walifikiri Isa alikuwa anamwambia akanunue vitu vilivyohitajika kwa ajili ya Sikukuu, au kuwapa maskini kitu. Mara tu baada ya kupokea ule mkate, Yuda akatoka nje. Wakati huo ulikuwa ni usiku.