Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 7:10-24

Yohana 7:10-24 NENO

Lakini ndugu zake walipokwisha kuondoka kwenda kwenye Sikukuu, yeye pia alienda lakini kwa siri. Viongozi wa Wayahudi walikuwa wakimtafuta huko kwenye Sikukuu na kuulizana, “Yuko wapi huyu mtu?” Kulikuwa na minong’ono iliyoenea kumhusu Isa katika umati wa watu, wakati wengine wakisema, “Ni mtu mwema.” Wengine walikuwa wakisema, “La, yeye anawadanganya watu.” Lakini hakuna mtu yeyote aliyemsema waziwazi kwa sababu ya kuwaogopa viongozi wa Wayahudi. Ilipokaribia katikati ya Sikukuu, Isa alipanda kwenda Hekaluni na kuanza kufundisha. Wayahudi wakastaajabia mafundisho yake wakasema, “Mtu huyu amepataje kujua mambo haya bila kufundishwa?” Ndipo Isa akawajibu, “Mafundisho yangu si yangu mwenyewe, bali yanatoka kwake yeye aliyenituma. Mtu yeyote akipenda kufanya mapenzi ya Mungu, atajua kama mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu au ninasema kwa ajili yangu mwenyewe. Wale wanenao kwa ajili yao wenyewe hufanya hivyo kwa kutaka utukufu wao wenyewe. Lakini yeye atafutaye utukufu wa yule aliyemtuma ni wa kweli, wala hakuna uongo ndani yake. Je, Musa hakuwapa ninyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja wenu anayeishika hiyo sheria. Kwa nini mnataka kuniua?” Ule umati wa watu wakamjibu, “Wewe una pepo mchafu! Ni nani anayetaka kukuua?” Isa akawajibu, “Nimefanya muujiza mmoja na nyote mkastaajabu. Lakini kwa kuwa Musa aliwaamuru tohara (ingawa kwa kweli haikutoka kwa Musa bali kwa baba zetu wa zamani), mnamtahiri mtoto hata siku ya Sabato. Ikiwa mtoto aweza kutahiriwa siku ya Sabato kusudi Torati ya Musa isivunjwe, kwa nini mnanikasirikia kwa kumponya mtu mwili wake wote siku ya Sabato? Acheni kuhukumu mambo kwa jinsi mnavyoona tu, bali hukumuni kwa haki.”