Ayubu 10
10
Ayubu anaendelea
1“Nayachukia sana haya maisha yangu;
kwa hiyo nitatoa malalamiko yangu kwa wazi bila kujizuia,
nami nitanena kutokana na uchungu wa moyo wangu.
2Nitamwambia Mungu: Usinihukumu,
bali niambie una mashtaka gani dhidi yangu.
3Je, inakupendeza wewe kunidhulumu,
kuikataa kazi ya mikono yako,
huku ukiunga mkono mipango ya waovu?
4Je, wewe una macho ya kimwili?
Je, wewe huona kama mwanadamu aonavyo?
5Je, siku zako ni kama zile za mwanadamu,
au miaka yako ni kama ile ya mtu,
6ili utafute makosa yangu
na kuichunguza dhambi yangu;
7ingawa unajua kuwa mimi sina hatia,
na hakuna awezaye kunitoa mkononi mwako?
8“Mikono yako ndiyo iliyoniumba na kunifanya.
Je, sasa utageuka na kuniangamiza?
9Kumbuka kuwa ulinifinyanga kama udongo wa mfinyanzi.
Je, sasa utanifanya kuwa mavumbi tena?
10Je, wewe hukunimimina mimi kama maziwa,
na kunigandisha kama jibini,
11ukanivika ngozi na nyama,
na kuniunga pamoja kwa mifupa na mishipa?
12Umenipa uhai na kunitendea wema,
katika uangalizi wako umeilinda roho yangu.
13“Lakini hili ndilo ulilolificha moyoni mwako,
nami ninajua kuwa hili lilikuwa katika nia yako:
14Kama nilifanya dhambi, ungekuwa umeniona,
wala usingeacha kosa langu lipite bila kuadhibiwa.
15Kama nina hatia, ole wangu!
Hata kama ningekuwa sina hatia,
siwezi kukiinua kichwa changu,
kwa kuwa nimejawa na aibu,
na kuzama katika mateso yangu.
16Nikiinua kichwa changu juu, unaniwinda kama simba,
na kuonesha tena uwezo wa kutisha dhidi yangu.
17Wewe waleta mashahidi wapya dhidi yangu
na kuzidisha hasira yako juu yangu;
nazo nguvu zako zinanijia wimbi moja baada ya jingine.
18“Kwa nini basi ulinitoa tumboni?
Ninatamani ningekufa kabla jicho lolote halijaniona.
19Laiti nisingezaliwa,
au kama ningepelekwa kaburini
moja kwa moja kutoka tumboni!
20Je, siku zangu chache si zimekaribia kwisha?
Niachie ili niweze kupata muda mfupi wa kufurahi
21kabla sijaenda mahali ambapo hakuna kurudi tena,
katika nchi ya giza na uvuli wa mauti,
22nchi ya giza nene sana,
yenye uvuli wa giza na machafuko,
ambapo hata nuru ni giza.”
Iliyochaguliwa sasa
Ayubu 10: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.