Ayubu 9
9
Hotuba ya tatu ya Ayubu
Ayubu anajibu: Hakuna Mpatanishi
1Kisha Ayubu akajibu:
2“Naam, najua hili ni kweli.
Lakini mwanadamu awezaje kuwa mwadilifu mbele za Mungu?
3Ingawa mtu angetaka kushindana naye,
hangeweza kumjibu Mungu hata mara moja miongoni mwa elfu moja.
4Hekima yake ni kubwa sana na ana uwezo mwingi mno.
Ni nani aliyempinga naye akawa salama?
5Aiondoa milima bila yenyewe kujua
na kuipindua kwa hasira yake.
6Aitikisa dunia kutoka mahali pake
na kuzifanya nguzo zake zitetemeke.
7Husema na jua, nalo likaacha kuangaza;
naye huizima mianga ya nyota.
8Yeye peke yake huzitandaza mbingu
na kuyakanyaga mawimbi ya bahari.
9Yeye ndiye Muumba wa nyota za Dubu#9:9 Dubu ni kundi la nyota za kaskazini; pia zinaitwa Dubu Mkuu., na Orioni#9:9 Orioni ni kundi la nyota kubwa.,
Kilimia#9:9 Kilimia ni kundi la nyota saba., na makundi ya nyota za kusini.
10Hutenda maajabu yasiyopimika,
miujiza isiyoweza kuhesabiwa.
11Anapopita karibu nami, siwezi kumwona;
apitapo mbele yangu, simtambui.
12Anapochukua kwa ghafula, ni nani awezaye kumzuia?
Ni nani awezaye kumwambia, ‘Unafanya nini?’
13Mungu hataizuia hasira yake;
hata jeshi kubwa la Rahabu#9:13 yaani Misri kwa fumbo lenye nguvu
linajikunyata miguuni pake.
14“Ni vipi basi mimi nitaweza kubishana naye?
Nawezaje kupata maneno ya kuhojiana naye?
15Ingawa sikuwa na hatia, sikuweza kumjibu;
ningeweza tu kumsihi Mhukumu wangu anihurumie.
16Hata kama ningemwita kwenye shauri, naye akakubali,
siamini kama angenisikiliza.
17Yeye angeniangamiza kwa dhoruba
na kuongeza majeraha yangu pasipo na sababu.
18Asingeniacha nipumue
bali angenifunika kabisa na huzuni kuu.
19Kama ni suala la nguvu, yeye ni mwenye nguvu!
Kama ni suala la haki, ni nani awezaye kumwita mahakamani?
20Hata kama sikuwa na hatia, kinywa changu kingenihukumu;
kama sikuwa na kosa, kingenitangaza kuwa mwenye hatia.
21“Ingawa mimi sina kosa,
haileti tofauti katika nafsi yangu;
nauchukia uhai wangu.
22Hayo yote ni sawa; ndiyo sababu nasema,
‘Yeye huwaangamiza wasio na makosa pamoja na waovu.’
23Wakati wa pigo liletapo kifo cha ghafula,
yeye hudhihaki kule kukata tamaa kwa yule asiye na kosa.
24Nchi inapoangukia mikononi mwa waovu,
yeye huwafunga macho mahakimu wake.
Kama si yeye, basi ni nani?
25“Siku zangu zapita mbio kuliko mkimbiaji;
zinapita upesi bila kuona furaha hata kidogo.
26Zinapita upesi kama mashua ya mafunjo,
mfano wa tai ayashukiaye mawindo kwa ghafula.
27Nikisema, ‘Nitayasahau malalamiko yangu,
nitabadili sura ya uso wangu na kutabasamu,’
28bado ninahofia mateso yangu yote,
kwa kuwa ninajua hutanihesabu kuwa sina hatia.
29Kwa kuwa nimeonekana mwenye hatia,
kwa nini basi nitaabishwe bure?
30Hata kama ningejiosha kwa sabuni
na kutakasa mikono yangu kwa magadi,
31wewe ungenitupa kwenye shimo la utelezi
kiasi kwamba hata nguo zangu zingenichukia sana.
32“Yeye si mwanadamu kama mimi ili niweze kumjibu,
ili tuweze kushindana naye mahakamani.
33Laiti pangekuwa na mtu wa kutupatanisha,
aweke mkono wake juu yetu sote wawili,
34mtu wa kuondoa fimbo ya Mungu juu yangu,
ili utisho wake usiendelee kunitia hofu.
35Ndipo ningenena naye, bila kumwogopa,
lakini kama ilivyo kwangu sasa, sitaweza.
Iliyochaguliwa sasa
Ayubu 9: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.