Ayubu 30
30
Ayubu anaendelea
1“Lakini sasa watu wadogo kwa umri kuliko mimi wananidhihaki,
watu ambao baba zao ningekataa kwa dharau
kuwaweka pamoja na mbwa wangu wa kulinda kondoo.
2Nguvu za mikono yao zingekuwa na faida gani kwangu,
kwa kuwa nguvu zao zilikuwa zimewaishia?
3Wakiwa wamekonda kutokana na kupungukiwa na kwa njaa,
walizurura usiku katika nchi kame iliyo ukiwa.
4Katika vichaka walikusanya mimea ya chumvi,
nacho chakula chao kilikuwa mizizi ya mti wa mfagio.
5Walifukuzwa mbali na watu wao,
wakipigiwa kelele kama wezi.
6Walilazimika kuishi katika mikondo ya vijito vilivyokauka,
kwenye majabali na mahandaki.
7Kwenye vichaka walilia kama punda,
na walijisongasonga pamoja kwenye vichaka.
8Wao ni watoto wa wapumbavu wenye asili ya ubaya,
waliofukuzwa watoke katika nchi.
9“Nao sasa wana wao wananidhihaki katika nyimbo;
nimekuwa kitu cha dhihaka kwao.
10Wananichukia sana na kujitenga nami,
wala hawasiti kunitemea mate usoni.
11Sasa kwa kuwa Mungu ameilegeza kamba ya upinde wangu na kunitesa,
wamekuwa huru kunitendea wanavyopenda.
12Kuume kwangu kundi linashambulia;
wao huitegea miguu yangu tanzi,
na kunizingira.
13Huizuia njia yangu,
nao hufanikiwa katika kuniletea maafa,
nami sina yeyote wa kunisaidia.
14Wananijia kama watu wapitao katika ufa mpana;
katikati ya magofu huja na kunishambulia.
15Vitisho vimenifunika;
heshima yangu imetoweshwa kama kwa upepo,
salama yangu imetoweka kama wingu.
16“Sasa maisha yangu yamefikia mwisho;
siku za mateso zimenikamata.
17Usiku mifupa yangu inachoma;
maumivu yanayonitafuna hayatulii kamwe.
18Kwa uwezo wake mkuu Mungu huwa kwangu kama nguo;
hushikamana nami kama ukosi wa vazi langu.
19Yeye amenitupa kwenye matope,
nami nimekuwa kama mavumbi na majivu.
20“Ee Mwenyezi Mungu, ninakulilia wewe lakini hunijibu;
ninasimama, nawe unanitazama tu.
21Wewe unanigeukia bila huruma;
unanishambulia kwa nguvu za mkono wako.
22Unaninyakua na kunipeperusha kwa upepo;
umenirusharusha kwenye dhoruba.
23Ninajua utanileta hadi kifoni,
mahali wenye uhai wote wamewekewa.
24“Hakika hakuna mtu anayemshambulia mhitaji
anapoomba msaada katika shida yake.
25Je, sikulia kwa ajili ya wale waliokuwa katika taabu?
Je, nafsi yangu haikusononeka kwa ajili ya maskini?
26Lakini nilipotazamia mema, mabaya yalinijia;
nilipotafuta nuru, ndipo giza lilipokuja.
27Kusukwasukwa ndani yangu kamwe hakutulii;
siku za mateso zinanikabili.
28Ninazunguka nikiwa nimeungua, lakini si kwa jua;
ninasimama katika kusanyiko nikiomba msaada.
29Nimekuwa ndugu wa mbweha,
rafiki wa mabundi.
30Ngozi yangu imekuwa nyeusi nayo inachunika;
mifupa yangu inaungua kwa homa.
31Kinubi changu kimegeuka kuwa maombolezo,
nayo filimbi yangu imekuwa sauti ya kilio.
Iliyochaguliwa sasa
Ayubu 30: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.