Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayubu 31

31
Ayubu anakamilisha maneno yake
1“Nimefanya agano na macho yangu
yasimtazame msichana kwa kumtamani.
2Kwa kuwa fungu la mwanadamu ni lipi kutoka kwa Mungu juu,
urithi wake kutoka juu kwa Mwenyezi?
3Je, si uharibifu kwa watu waovu,
maangamizi kwa wale watendao mabaya?
4Je, yeye hazioni njia zangu
na kuihesabu kila hatua yangu?
5“Kama nimeishi katika uongo
au mguu wangu umekimbilia udanganyifu,
6Mungu na anipime katika mizani za uaminifu,
naye atajua kwamba sina hatia:
7kama hatua zangu zimepotoka kutoka njia,
kama moyo wangu umeongozwa na macho yangu,
au kama mikono yangu imetiwa unajisi,
8basi wengine na wale nilichokipanda,
nayo yale yote niliyootesha na yang’olewe.
9“Kama moyo wangu umeshawishiwa na mwanamke,
au kama nimevizia mlangoni mwa jirani yangu,
10basi mke wangu na asage nafaka ya mwanaume mwingine,
nao wanaume wengine walale naye.
11Kwa kuwa hilo lingekuwa aibu,
naam, dhambi ya kuhukumiwa.
12Ni moto uwakao kwa Uharibifu#31:12 Kwa Kiebrania ni Abadon (Ayubu 26:6; Mithali 15:11).;
ungekuwa umeng’oa mavuno yangu.
13“Kama ningewanyima haki watumishi wangu wanaume au vijakazi wangu,
walipokuwa na manung’uniko dhidi yangu,
14nitafanya nini Mungu atakaponikabili?
Nitamjibu nini nitakapoitwa kujitetea?
15Je, yeye aliyeniumba tumboni mwa mama yangu,
siye aliyewaumba?
Je, si ni yeye huyo mmoja aliyetuumba sote
ndani ya mama zetu?
16“Ikiwa nimewanyima maskini haja zao,
au kuyaacha macho ya wajane yadhoofike,
17kama nimekula chakula changu mwenyewe,
bila kuwashirikisha yatima;
18lakini tangu ujana wangu nimemlea yatima kama ambavyo baba angefanya,
nami tangu kuzaliwa kwangu nimewaongoza wajane:
19kama nilimwona yeyote akiteseka kwa kukosa nguo,
au mtu mhitaji asiye na mavazi,
20ambaye wala moyo wake haukunibariki
kwa kumpatia joto kwa mavazi ya manyoya ya kondoo wangu,
21na kama nimeinua mkono wangu dhidi ya yatima,
nikijua kuwa nina ushawishi mahakamani,
22basi mkono wangu na unyofoke toka begani mwangu,
nao na uvunjike kutoka kiungio chake.
23Kwa kuwa niliogopa uharibifu kutoka kwa Mungu,
nami kwa kuuogopa utukufu wake sikuweza kufanya mambo kama hayo.
24“Kama nimeweka tumaini langu kwenye dhahabu,
au kuiambia dhahabu safi, ‘Wewe ndiwe salama yangu,’
25kama nimefurahia wingi wa utajiri wangu,
ustawi ambao mikono yangu ilikuwa imepata,
26kama nimelitazama jua katika kung’aa kwake
au mwezi ukienda kwa fahari yake,
27hivyo moyo wangu kushawishiwa kwa siri,
au kubusu mkono wangu kwa kuviheshimu,
28basi hiyo pia ingekuwa dhambi ya kuhukumiwa,
kwa kuwa ningekuwa si mwaminifu kwa Mungu aishiye juu sana.
29“Kama nimeshangilia msiba wa adui yangu,
au kutazama kwa furaha taabu iliyomjia,
30lakini sikuruhusu kinywa changu kufanya dhambi
kwa kuomba laana dhidi ya maisha yake;
31kama watu wa nyumbani mwangu kamwe hawakusema,
‘Ni nani ambaye hajashibishwa na nyama ya Ayubu?’
32Lakini hakuna mgeni aliyelala njiani,
kwa maana mlango wangu ulikuwa wazi kwa msafiri;
33kama nimeifunika dhambi yangu kama wanadamu wengine wafanyavyo,
kwa kuficha hatia yangu moyoni mwangu,
34kwa sababu ya kuogopa umati wa watu,
na hivyo kuwa na hofu ya kudharauliwa na jamaa,
nikakaa kimya, nisitoke nje ya mlango.
35(“Laiti angekuwepo mtu wa kunisikia!
Tazama sasa ninatia sahihi kwenye utetezi wangu:
Mwenyezi na anijibu;
mshtaki wangu na aweke mashtaka yake kwenye maandishi.
36Hakika ningeyavaa begani mwangu,
ningeyavaa kama taji.
37Ningempa hesabu ya kila hatua yangu,
ningemwendea kama mwana wa mfalme.)
38“Kama nchi yangu inalia dhidi yangu,
na mifereji yake yote imelowana kwa machozi,
39kama nimekula mazao yake bila malipo,
au kuvunja mioyo ya wapangaji wake,
40basi miiba na iote badala ya ngano,
na magugu badala ya shayiri.”
Mwisho wa maneno ya Ayubu.

Iliyochaguliwa sasa

Ayubu 31: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia