Ayubu 33:23-33
Ayubu 33:23-33 NEN
“Kama bado kuna malaika upande wake kama mtetezi, mmoja miongoni mwa elfu, wa kumwambia mwanadamu lililo jema kwake, kumwonea huruma na kusema, ‘Mwokoe asije akatumbukia shimoni; nimepata ukombozi kwa ajili yake’: ndipo nyama ya mwili wake hufanywa mpya kama ya mtoto; hurudishwa upya kama siku za ujana wake. Humwomba Mungu, akapata kibali kwake, huuona uso wa Mungu na kushangilia kwa furaha; Mungu humrudisha katika hali yake ya uadilifu. Ndipo huja mbele za watu na kusema, ‘Nilitenda dhambi na kupotosha kilichokuwa haki, lakini sikuadhibiwa kama nilivyostahili. Alinikomboa nafsi yangu nisitumbukie shimoni, nami nitaishi ili kuufurahia mwanga.’ “Mungu hufanya haya yote kwa mwanadamu; mara mbili hata mara tatu, ili aigeuze nafsi yake toka shimoni, ili nuru ya uzima imwangazie. “Ayubu, zingatia, nisikilize mimi; nyamaza, nami nitanena. Kama unalo lolote la kusema, unijibu; sema, kwa maana ninataka uonekane huna hatia. Lakini kama huna la kusema, basi nisikilize mimi; nyamaza, nami nitakufundisha hekima.”