Ayubu 39:1-12
Ayubu 39:1-12 NEN
“Je, wajua ni wakati gani mbuzi wa mlimani wanapozaa? Je, watambua ni wakati gani kulungu jike azaapo mtoto wake? Je, waweza kuhesabu miezi hadi wazaapo? Je, unajua majira yao ya kuzaa? Wao hujiinamisha na kuzaa watoto wao; utungu wa kuzaa unakoma. Watoto wao hustawi na kuongezeka nguvu nyikani; huenda zao wala hawarudi tena. “Ni nani aliyemwachia punda-mwitu awe huru? Ni nani aliyezifungua kamba zake? Nimempa nchi isiyokaliwa na watu kuwa masikani yake, nchi ya chumvi kuwa makao yake. Huzicheka ghasia za mji, wala hasikii kelele za mwendesha gari. Huzunguka vilimani kwa ajili ya malisho na kutafuta kila kitu kibichi. “Je, nyati atakubali kukutumikia? Atakaa karibu na hori lako usiku? Je, waweza kumfungia kwenye matuta kwa kamba? Je, atalima mabonde nyuma yako? Je, utamtumainia kwa ajili ya nguvu zake nyingi? Utamwachia yeye kazi zako nzito? Utaweza kumwamini akuletee nafaka yako nyumbani kutoka shambani na kuikusanya kwenye sakafu yako ya kupuria?