Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayubu Utangulizi

Utangulizi
Kitabu hiki kimepewa jina la mhusika wake mkuu ambaye ni Ayubu. Ayubu alikuwa ni mtu tajiri na mwenye haki mbele za Mwenyezi Mungu. Maana ya jina Ayubu ni “Yule anayemrudia Mwenyezi Mungu daima”. Hata baada ya kuondokewa na vitu vyote na kuugua majipu yaliyomletea maumivu na mateso makali mwilini, Ayubu bado alikiri kumpenda Mwenyezi Mungu. Lakini rafiki zake Ayubu walisisitiza kwamba alikuwa anateseka kwa sababu alikuwa ametenda dhambi, na kwamba hiyo ilikuwa ni adhabu yake. Ayubu alijitetea kwa kusisitiza kwamba hajafanya uovu ambao ungemsababishia hiyo adhabu na kwamba yeye anamwamini Mwenyezi Mungu. Ndipo Mwenyezi Mungu alipozungumza na kuonesha uwezo wake mkubwa. Mwishowe, Ayubu alikiri kwamba Mwenyezi Mungu ni mkuu na wa ajabu kwetu, kiasi kwamba hatuwezi kumwelewa.
Mwandishi
Haijulikani kwa dhahiri ni nani aliyekiandika kitabu hiki; huenda ikawa ni Ayubu. Wengine hudhani ni Musa, Sulemani au Elihu.
Kusudi
Kitabu hiki kinaonesha mateso ya mwenye haki, uweza na uaminifu wa Mwenyezi Mungu, na pia kinathibitisha maana ya imani ya kweli ya mtu wa Mwenyezi Mungu. Kitabu hiki kinaonesha baraka zinazoambatana na ushindi baada ya majaribu. Kwa hiyo kazi ya majaribu ambayo Mwenyezi Mungu anayaruhusu ni kututhibitisha katika imani. Kitabu hiki kinazungumzia swali hili: “Ni kwa nini wenye haki huteseka?”
Mahali
Inadhaniwa kuwa kitabu cha Ayubu kiliandikwa katika nchi ya Usi. Nchi hii ilikuwa kaskazini mashariki mwa Palestina, karibu na jangwa lililo kati ya Dameski na Mto Frati.
Tarehe
Tarehe ya kuandikwa kwa kitabu hiki haijulikani; kinadhaniwa kuwa kitabu cha zamani sana kuliko vingine vyote katika Maandiko Matakatifu. Yawezekana kuwa mambo yalioandikwa kwenye kitabu hiki yalitukia mnamo 2000–1800 K.K.
Wahusika Wakuu
Ayubu, Elifazi Mtemani, Bildadi Mshuhi, Sofari Mnaamathi, na Elihu wa kabila la Buzi.
Wazo Kuu
Mwenyezi Mungu ametuwekea ugo pande zote. Hivyo Shetani hawezi kutushambulia bila Mwenyezi Mungu kujua, lakini wakati mwingine Mwenyezi Mungu hutoa ruhusa ili kumthibitishia adui juu ya uelekevu na uadilifu wa mtu wake. Hivyo basi, kumtumaini Mwenyezi Mungu wakati wote na katika hali zote huleta ushindi dhidi ya Shetani.
Mambo Muhimu
Kujaribiwa kwa Ayubu, mazungumzo kati ya Ayubu na rafiki zake watatu, na majibu ya Mwenyezi Mungu kwa Ayubu yaliyoambatana na baraka ya watoto na mali nyingi kwa Ayubu.
Yaliyomo
Sehemu ya kwanza: Habari za awali, na Ayubu kujaribiwa (1:1–2:13)
Sehemu ya pili: Mazungumzo ya Ayubu na rafiki zake watatu (3:1–31:40)
Mwenyezi Mungu anahusikaje na mateso ya Ayubu? (3:1–14:22)
Je, watu waovu huwa wanateseka mara zote? (15:1–21:34)
Je, Ayubu ana hatia ya kuwa na dhambi ya siri? (22:1–31:40)
Sehemu ya tatu: Mazungumzo ya Elihu (32:1–37:24)
Sehemu ya nne: Mwenyezi Mungu amjibu Ayubu (38:1–41:34)
Sehemu ya tano: Ayubu amjibu Mwenyezi Mungu, na Mwisho (42:1-17).

Iliyochaguliwa sasa

Ayubu Utangulizi: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia