Yoeli 1:1-12
Yoeli 1:1-12 NENO
Neno la Mwenyezi Mungu ambalo lilimjia Yoeli mwana wa Pethueli. Sikilizeni hili, enyi wazee; sikilizeni, ninyi nyote mnaoishi katika nchi. Je, jambo kama hili lilishawahi kutokea katika siku zenu au katika siku za babu zenu? Waelezeni watoto wenu, na watoto wenu wawaambie watoto wao, na watoto wao kwa kizazi kitakachofuata. Kilichosazwa na kundi la tunutu nzige wakubwa wamekula, kilichosazwa na nzige wakubwa parare wamekula, kilichosazwa na parare madumadu wamekula. Amkeni, enyi walevi, mlie! Pigeni yowe enyi wanywaji wote wa mvinyo, pigeni yowe kwa sababu ya mvinyo mpya, kwa kuwa mmenyang’anywa kutoka midomoni mwenu. Taifa limevamia nchi yangu, lenye nguvu tena lisilo na idadi; lina meno ya simba, magego ya simba jike. Limeharibu mizabibu yangu na kuangamiza mitini yangu. Limebambua magome yake na kuyatupilia mbali, likayaacha matawi yake yakiwa meupe. Omboleza kama bikira aliyevaa gunia akimwomboleza mume wa ujana wake. Sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji zimekatiliwa mbali kutoka nyumba ya Mwenyezi Mungu. Makuhani wanaomboleza, wale wanaohudumu mbele za Mwenyezi Mungu. Mashamba yameharibiwa, ardhi imekauka; nafaka imeharibiwa, mvinyo mpya umekauka, mafuta yamekoma. Kateni tamaa, enyi wakulima, lieni, enyi mlimao mizabibu; huzunikeni kwa ajili ya ngano na shayiri, kwa sababu mavuno ya shambani yameharibiwa. Mzabibu umekauka na mtini umenyauka; mkomamanga, mtende na mtofaa, miti yote shambani, imekauka. Hakika furaha yote ya mwanadamu imeondoka.