Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoeli 1:1-12

Yoeli 1:1-12 SRUV

Neno la BWANA lililomjia Yoeli, mwana wa Pethueli. Sikieni haya, enyi wazee; Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi. Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu, Au katika siku za baba zenu? Waambieni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine. Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu. Levukeni, enyi walevi, mkalie; Pigeni yowe, ninyi nyote mnywao divai; Kwa sababu ya divai mpya; Maana umekatiliwa mbali na vinywa vyenu. Maana taifa limepanda juu ya nchi yangu, Lenye nguvu, tena halina hesabu; Meno yake ni kama meno ya simba, Naye ana magego ya simba mkubwa. Ameuharibu mzabibu wangu; ameuvunja mtini wangu; ameyaambua magamba yake kabisa; ameuangusha chini; matawi yake yamefanywa kuwa meupe. Omboleza kama mwanamwali avaaye magunia Kwa ajili ya mume wa ujana wake. Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimekatiliwa mbali na nyumba ya BWANA; Hao makuhani, wahudumu wa BWANA, wanaomboleza. Shamba limeharibika, nchi inaomboleza; maana nafaka imeharibika, divai mpya imekauka, mafuta yamepunguka. Tahayarini, enyi wakulima; Pigeni yowe, enyi watunzaji wa mizabibu; Kwa ajili ya ngano na shayiri, Maana mavuno ya mashamba yamepotea. Mzabibu umesinyaa, mtini nao umevia; Nao mkomamanga na mtende na mtofaa; Naam, miti yote ya mashamba imekauka; Maana furaha imetoweka kwa wanadamu.

Soma Yoeli 1