Yona 3
3
Yona aenda Ninawi
1Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yona mara ya pili: 2“Ondoka uende katika mji mkubwa wa Ninawi, ukautangazie ujumbe ninaokupa.”
3Yona akalitii neno la Mwenyezi Mungu naye akaenda Ninawi. Basi Ninawi ulikuwa mji maarufu sana, ilichukua siku tatu kuuzunguka. 4Siku ya kwanza, Yona aliingia mjini. Akatangaza: “Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa.” 5Watu wa Ninawi wakamwamini Mungu, wakatangaza kufunga, watu wote kuanzia mkubwa sana hadi yule mdogo kabisa, wakavaa gunia.
6Habari zilipomfikia mfalme wa Ninawi, aliondoka kwenye kiti chake cha utawala, akavua majoho yake ya mfalme, akajifunika gunia na kuketi mavumbini. 7Ndipo akatoa tangazo katika Ninawi yote:
“Kwa amri ya mfalme na wakuu wake:
“Msiruhusu mtu yeyote au mnyama, makundi ya ng’ombe au wanyama wengine wafugwao, kuonja kitu chochote, msiwaruhusu kula wala kunywa. 8Bali wanadamu na wanyama wavae gunia. Kila mmoja afanye hima kumwomba Mungu. Waziache njia zao mbaya na udhalimu ulio mikononi mwao. 9Ni nani ajuaye? Huenda Mungu akaghairi kwa huruma yake akaacha hasira yake kali ili tusiangamie.”
10Mungu alipoona walivyofanya na jinsi walivyogeuka kutoka njia zao mbaya, akawa na huruma wala hakuleta maangamizi juu yao kama alivyokuwa ameonya.
Iliyochaguliwa sasa
Yona 3: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.