Yona 4
4
Hasira ya Yona kwa ajili ya huruma ya Mwenyezi Mungu
1Lakini Yona alichukizwa sana akakasirika. 2Akamwomba Mwenyezi Mungu, “Ee Mwenyezi Mungu, hili si lile nililolisema nilipokuwa ningali nyumbani? Hii ndiyo sababu niliharakisha kukimbilia Tarshishi. Nikifahamu kuwa wewe ni Mungu mwenye neema na huruma, si mwepesi wa hasira na umejaa upendo, ni Mungu ambaye hughairi katika kupeleka maafa. 3Sasa, Ee Mwenyezi Mungu, niondolee uhai wangu, kwa kuwa ni afadhali mimi nife kuliko kuishi.”
4Lakini Mwenyezi Mungu akamjibu, “Je unayo haki yoyote kukasirika?”
5Yona akatoka nje akaketi mahali upande wa mashariki wa mji. Hapo akajitengenezea kibanda, akaketi kwenye kivuli chake na kungojea ni nini kitakachotokea katika mji. 6Ndipo Bwana Mwenyezi Mungu akaweka tayari mzabibu na kuufanya uote, kumpa Yona kivuli kilichomfunika kichwa ili kuondoa taabu yake, naye Yona akafurahi sana kwa ajili ya ule mzabibu. 7Lakini kesho yake asubuhi na mapema Mungu akaamuru buu, autafune mzabibu huo nao ukanyauka. 8Jua lilipochomoza, Mungu akautuma upepo wa hari wa mashariki, nalo jua likawaka juu ya kichwa cha Yona hadi akazimia. Akatamani kufa, naye akasema, “Ni afadhali mimi nife kuliko kuishi.”
9Lakini Mungu alimwambia Yona, “Je, unayo haki kukasirika kuhusu mzabibu huo?”
Akasema, “Ndiyo, ninayo haki. Nimekasirika kiasi cha kufa.”
10Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia, “Wewe unakasirika kwa ajili ya mzabibu huu, nawe hukuusababisha kuota wala kuutunza. Uliota usiku mmoja, nao ukafa usiku mmoja. 11Lakini Ninawi ina zaidi ya watu elfu mia moja na ishirini ambao hawawezi kupambanua kulia au kushoto, pamoja na ng’ombe wengi. Je, hainipasi kufikiri kuhusu mji ule mkubwa?”
Iliyochaguliwa sasa
Yona 4: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.