Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Maombolezo 5:1-22

Maombolezo 5:1-22 NEN

Kumbuka, Ee BWANA, yaliyotupata, tazama, nawe uione aibu yetu. Urithi wetu umegeuziwa kwa wageni, na nyumba zetu kwa wageni. Tumekuwa yatima wasio na baba, mama zetu wamekuwa kama wajane. Ni lazima tununue maji tunayokunywa, kuni zetu zapatikana tu kwa kununua. Wanaotufuatilia wapo kwenye visigino vyetu, tumechoka na hakuna pumziko. Tumejitolea kwa Misri na Ashuru tupate chakula cha kutosha. Baba zetu walitenda dhambi na hawapo tena, na sisi tunachukua adhabu yao. Watumwa wanatutawala na hakuna wa kutuokoa mikononi yao. Tunapata chakula chetu kwa kuhatarisha maisha yetu kwa sababu ya upanga jangwani. Ngozi yetu ina joto kama tanuru, kwa sababu ya fadhaa itokanayo na njaa. Wanawake wametendwa jeuri katika Sayuni, na mabikira katika miji ya Yuda. Wakuu wametungikwa juu kwa mikono yao, wazee hawapewi heshima. Vijana wanataabika kwenye mawe ya kusagia, wavulana wanayumbayumba chini ya mizigo ya kuni. Wazee wameondoka langoni la mji, vijana wameacha kuimba nyimbo zao. Furaha imeondoka mioyoni mwetu, kucheza kwetu kumegeuka maombolezo. Taji imeanguka kutoka kichwani petu. Ole wetu, kwa maana tumetenda dhambi! Kwa sababu hiyo, mioyo yetu inazimia, kwa sababu ya hayo, macho yetu yamefifia, kwa ajili ya Mlima Sayuni, ambao unakaa ukiwa, nao mbweha wanatembea juu yake. Wewe, Ee BWANA unatawala milele, kiti chako cha enzi chadumu kizazi hadi kizazi. Kwa nini watusahau siku zote? Kwa nini umetuacha kwa muda mrefu? Turudishe kwako mwenyewe, Ee BWANA, ili tupate kurudi. Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale, isipokuwa uwe umetukataa kabisa na umetukasirikia pasipo kipimo.