Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Omb 5:1-22

Omb 5:1-22 SUV

Ee BWANA, kumbuka yaliyotupata; Utazame na kuiona aibu yetu. Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni; Na nyumba zetu kuwa mali ya makafiri. Tumekuwa yatima waliofiwa na baba; Mama zetu wamekuwa kama wajane. Tumekunywa maji yetu kwa fedha; Kuni zetu twauziwa. Watufuatiao wa juu ya shingo zetu; Tumechoka tusipate raha yo yote. Tumewapa hao Wamisri mkono; Na Waashuri nao, ili tushibe chakula. Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao. Watumwa wanatutawala; Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao. Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu; Kwa sababu ya upanga wa nyikani. Ngozi yetu ni nyeusi kama tanuu; Kwa sababu ya hari ya njaa ituteketezayo. Huwatia jeuri wanawake katika Sayuni; Na mabikira katika miji ya Yuda. Wakuu hutungikwa kwa mikono yao; Nyuso za wazee hazipewi heshima. Vijana huyachukua mawe ya kusagia; Na watoto hujikwaa chini ya kuni. Wazee wameacha kwenda langoni; Na vijana kwenda ngomani. Furaha ya mioyo yetu imekoma; Machezo yetu yamegeuka maombolezo. Taji ya kichwa chetu imeanguka; Ole wetu! Kwa kuwa tumetenda dhambi. Kwa sababu hiyo mioyo yetu imezimia; Kwa ajili ya hayo macho yetu hayaoni vema. Kwa ajili ya mlima Sayuni ulio ukiwa, Mbweha hutembea juu yake. Wewe, BWANA, unadumu milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi. Mbona watusahau sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi? Ee BWANA, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale. Isipokuwa wewe umetukataa kabisa; Nawe una hasira nyingi sana juu yetu.