Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 22:26-38

Luka 22:26-38 NENO

Lakini ninyi msifanane nao. Bali yeye aliye mkuu kuliko wote miongoni mwenu, inampasa kuwa kama yeye aliye mdogo wa wote, naye anayetawala na awe kama yeye anayehudumu. Kwani ni nani aliye mkuu? Ni yule anayeketi mezani au ni yule anayehudumu? Si ni yule aliyeketi mezani? Lakini mimi niko miongoni mwenu kama yule anayehudumu. Ninyi mmekuwa pamoja nami katika majaribu yangu. Nami kama Baba yangu alivyonipa ufalme, nami ninawapa ninyi, ili mpate kula na kunywa mezani pangu katika karamu ya ufalme wangu, na kukaa katika viti vya utawala, mkihukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.” Isa akasema, “Simoni, Simoni, sikiliza, Shetani ameomba kuwapepeta ninyi wote kama ngano. Lakini nimekuombea wewe Simoni ili imani yako isishindwe, nawe baada ya kunirudia, uwaimarishe ndugu zako.” Petro akajibu, “Bwana, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata katika kifo.” Isa akamjibu, “Ninakuambia Petro, kabla jogoo hajawika usiku wa leo, utakana mara tatu kwamba unanijua.” Kisha Isa akawauliza, “Nilipowatuma bila mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu chochote?” Wakajibu, “La, hatukupungukiwa na kitu chochote.” Akawaambia, “Lakini sasa, aliye na mfuko na auchukue, na aliye na mkoba vivyo hivyo. Naye asiye na upanga, auze joho lake anunue mmoja. Kwa sababu, nawaambia, andiko hili lazima litimizwe kunihusu, kwamba, ‘Alihesabiwa pamoja na wakosaji’; kwa kweli yaliyoandikwa kunihusu hayana budi kutimizwa.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, tazama hapa kuna panga mbili.” Akawajibu, “Inatosha.”