Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 13:1-17

Mathayo 13:1-17 NEN

Siku iyo hiyo Yesu akatoka nje ya nyumba, akaketi kando ya bahari. Umati mkubwa mno wa watu ukakusanyika kumzunguka, hata ikabidi aingie katika chombo na kuketi humo, nao watu wote wakawa wamesimama ukingoni mwa bahari. Ndipo akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema: “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila. Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba. Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina. Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea. Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri ambapo zilitoa mazao, nyingine mara mia moja, nyingine mara sitini, na nyingine mara thelathini. Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.” Wanafunzi wake wakamwendea, wakamuuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?” Akawajibu, “Ninyi mmepewa kuzifahamu siri za Ufalme wa Mbinguni, lakini wao hawajapewa. Kwa maana yule aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyangʼanywa. Hii ndiyo sababu nasema nao kwa mifano: “Ingawa wanatazama, hawaoni; wanasikiliza, lakini hawasikii, wala hawaelewi. Kwao unatimia ule unabii wa Isaya aliposema: “ ‘Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa; na pia mtatazama lakini hamtaona. Kwa kuwa mioyo ya watu hawa imekuwa migumu; hawasikii kwa masikio yao, na wamefumba macho yao. Wasije wakaona kwa macho yao, na wakasikiliza kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, na kugeuka nami nikawaponya.’ Lakini heri macho yenu kwa sababu yanaona, na heri masikio yenu kwa sababu yanasikia. Amin, nawaambia, manabii wengi na wenye haki walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mathayo 13:1-17