Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 24:15-35

Mathayo 24:15-35 NENO

“Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu (asomaye na afahamu), basi wale walio Yudea wakimbilie milimani. Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke ili kuchukua chochote kutoka ndani ya nyumba. Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake. Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato. Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwepo tangu mwanzo wa dunia hadi sasa: wala haitakuwepo tena kamwe. “Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna mtu ambaye angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, siku hizo zitafupishwa. Wakati huo mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ au, ‘Kristo yuko kule,’ msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa. Tazameni, nimekwisha kuwaambia mapema. “Basi mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki. Kwa maana kama vile radi itokavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa maana popote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai. “Mara baada ya dhiki ya siku zile, “ ‘jua litatiwa giza, nao mwezi hautatoa nuru yake; nazo nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za anga zitatikisika.’ “Ndipo itakapotokea ishara ya Mwana wa Adamu angani, na makabila yote ya dunia yataomboleza. Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya angani, katika uwezo na utukufu mkuu. Naye atawatuma malaika wake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine. “Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. Vivyo hivyo, mnapoyaona mambo haya yote, mtambue kwamba wakati u karibu, hata malangoni. Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.