Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 26:36-45

Mathayo 26:36-45 NEN

Kisha Yesu akaenda pamoja na wanafunzi wake mpaka kwenye bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia, “Kaeni hapa, nami niende kule nikaombe.” Akamchukua Petro pamoja na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kufadhaika. Kisha Yesu akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.” Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.” Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamuuliza Petro, “Je, ninyi hamkuweza kukesha pamoja nami hata kwa saa moja? Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.” Akaenda tena mara ya pili na kuomba, “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, basi mapenzi yako yafanyike.” Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. Hivyo akawaacha akaenda zake tena mara ya tatu na kuomba akisema maneno yale yale. Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Tazameni, saa imefika ambapo Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi.