Mathayo 27:27-44
Mathayo 27:27-44 NENO
Kisha askari wa mtawala wakampeleka Isa kwenye Praitorio, na wakakusanya kikosi kizima cha askari kumzunguka. Wakamvua nguo zake na kumvika vazi la rangi nyekundu, kisha wakasokota taji la miiba, wakaiweka kichwani pake. Wakamwekea fimbo katika mkono wake wa kuume, na wakapiga magoti mbele zake na kumdhihaki, wakisema, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” Wakamtemea mate, wakachukua ile fimbo wakampiga kichwani tena na tena. Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakampeleka ili wakamsulubishe. Walipokuwa wakienda, wakakutana na mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba. Wakafika mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa). Hapo wakampa Isa divai iliyochanganywa na nyongo ili anywe; lakini alipoionja, akakataa kuinywa. Walipokwisha kumsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. [Hili lilifanyika ili litimie neno lililonenwa na nabii, “Waligawa nguo zangu miongoni mwao na vazi langu wakalipigia kura.”] Kisha wakaketi, wakamchunga. Juu ya kichwa chake, kwenye msalaba, wakaandika shtaka lake hivi: HUYU NI ISA MFALME WA WAYAHUDI. Wanyang’anyi wawili walisulubiwa pamoja naye, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao, na kusema, “Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe basi! Kama wewe ni Mwana wa Mungu, shuka msalabani.” Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani, walimu wa Torati pamoja na wazee wakamdhihaki, wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Yeye ni mfalme wa Israeli! Ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Anamwamini Mungu, basi Mungu na amwokoe sasa kama anamtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’ ” Hata wale wanyang’anyi waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana vivyo hivyo.