Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mika 1

1
1Neno la Mwenyezi Mungu lilimjia Mika Mmoreshethi wakati wa utawala wa Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, ufunuo aliouona kuhusu Samaria na Yerusalemu.
2Sikieni, enyi mataifa, enyi nyote,
sikilizeni, ee dunia na wote mliomo,
ili Bwana Mungu Mwenyezi ashuhudie dhidi yenu,
Bwana kutoka Hekalu lake takatifu.
Hukumu dhidi ya Samaria na Yerusalemu
3Tazama! Mwenyezi Mungu anakuja kutoka mahali pake;
anashuka na kukanyaga
mahali palipoinuka juu pa dunia.
4Milima inayeyuka chini yake
na mabonde yanagawanyika
kama nta mbele ya moto,
kama maji yanayotiririka kasi
kwenye mteremko.
5Yote haya ni kwa sababu ya kosa la Yakobo,
ni kwa sababu ya dhambi za nyumba ya Israeli.
Kosa la Yakobo ni lipi?
Je, sio Samaria?
Je, mahali pa juu pa Yuda pa kuabudia ni nini?
Je, sio Yerusalemu?
6“Kwa hiyo nitaufanya Samaria kuwa lundo la kokoto,
mahali pa kuotesha mizabibu.
Nitayamwaga mawe yake katika bonde
na kuacha wazi misingi yake.
7Sanamu zake zote
zitavunjwa vipande vipande;
zawadi zake zote za Hekalu
zitachomwa kwa moto;
nitaharibu vinyago vyake vyote.
Kwa kuwa alikusanya zawadi zake
kutokana na ujira wa kahaba,
nazo zitatumika tena
kulipa mishahara ya kahaba.”
Kulia na kuomboleza
8Kwa ajili ya hili nitalia na kuomboleza;
nitatembea bila viatu na tena uchi.
Nitabweka kama mbweha
na kuomboleza kama bundi.
9Kwa sababu jeraha lake halitibiki;
limekuja kwa Yuda.
Limefika hasa kwenye lango la watu wangu,
hata Yerusalemu kwenyewe.
10Usiliseme hili huko Gathi;
usilie hata kidogo.
Huko Beth-le-Afra
gaagaa mavumbini.
11Piteni mkiwa uchi na wenye aibu,
ninyi mnaoishi Shafiri.
Wale wanaoishi Saanani
hawatatoka nje.
Beth-Eseli iko katika maombolezo;
kinga yake imeondolewa kwako.
12Wale wanaoishi Marothi wanagaagaa kwa maumivu
wakingoja msaada,
kwa sababu maangamizi yamekuja
kutoka kwa Mwenyezi Mungu,
hata katika lango la Yerusalemu.
13Enyi mnaoishi Lakishi,
fungeni farasi kwenye magari ya vita.
Mlikuwa chanzo cha dhambi
kwa Binti Sayuni,
kwa kuwa makosa ya Israeli
yalikutwa kwako.
14Kwa hiyo utaipa Moresheth-Gathi
zawadi za kuagana.
Mji wa Akzibu utaonesha wazi udanganyifu
kwa wafalme wa Israeli.
15Nitawaleteeni atakayewashinda
ninyi mnaoishi Maresha.
Yeye aliye utukufu wa Israeli
atakuja Adulamu.
16Nyoeni nywele zenu katika kuomboleza
kwa ajili ya watoto wenu mnaowafurahia;
jifanyieni upara kama tai,
kwa kuwa watawaacha
na kwenda uhamishoni.

Iliyochaguliwa sasa

Mika 1: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia