Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 16

16
Isa afufuka
(Mathayo 28:1-8; Luka 24:1-12; Yohana 20:1-10)
1Sabato ilipomalizika, Mariamu Magdalene, Mariamu mama yake Yakobo, na Salome walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Isa. 2Asubuhi na mapema, siku ya kwanza ya juma, mara tu baada ya kuchomoza jua, walienda kaburini. 3Njiani wakawa wanaulizana wao kwa wao, “Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe kutoka ingilio la kaburi?”
4Lakini walipotazama, wakaona lile jiwe, ambalo lilikuwa kubwa sana, limekwisha kuvingirishwa kutoka pale penye ingilio la kaburi. 5Walipokuwa wakiingia mle kaburini, wakamwona kijana mmoja aliyevaa joho jeupe akiwa ameketi upande wa kuume, nao wakastaajabu.
6Yule malaika akawaambia, “Msistaajabu. Mnamtafuta Isa, Mnasiri, aliyesulubiwa. Amefufuka! Hayuko hapa. Tazameni mahali walipomlaza. 7Lakini nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro, kwamba, ‘Anawatangulia kwenda Galilaya. Mtamwona huko kama alivyowaambia.’ ”
8Hivyo wakatoka, wakakimbia kutoka mle kaburini wakiwa na hofu kuu na mshangao. Nao hawakumwambia mtu yeyote neno lolote, kwa sababu waliogopa.
Isa amtokea Mariamu Magdalene
(Mathayo 28:9-10; Yohana 20:11-18)
[ 9#16:9 Maandiko mengine ya kale hayana sehemu ya Marko 16:9-20. Isa alipofufuka alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, aliyekuwa amemtoa pepo wachafu saba. 10Mariamu akaenda, naye akawaambia wale waliokuwa wamefuatana na Isa, waliokuwa wanaomboleza na kulia. 11Lakini waliposikia kwamba Isa yu hai na kwamba Mariamu alikuwa amemwona, hawakusadiki.
Isa awatokea wanafunzi wawili
(Luka 24:13-35)
12Baadaye Isa akawatokea wawili miongoni mwa wanafunzi wake walipokuwa wakienda shambani akiwa katika sura nyingine. 13Nao wakarudi na kuwaambia wenzao. Lakini hawakuwasadiki wao pia.
Isa awatuma wanafunzi wake
(Mathayo 28:16-20; Luka 24:36-49; Yohana 20:19-23; Matendo 1:6-8)
14Baadaye Isa akawatokea wale wanafunzi kumi na mmoja walipokuwa wakila chakula. Akawakemea kwa kutoamini kwao na kwa ugumu wa mioyo yao kwa kutosadiki wale waliomwona baada yake kufufuka.
15Akawaambia, “Nendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. 16Yeyote aaminiye na kubatizwa#16:16 Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali. ataokoka. Lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa. 17Nazo ishara hizi zitafuatana na wanaoamini: Kwa Jina langu watatoa pepo wachafu; watasema kwa lugha mpya; 18watashika nyoka kwa mikono yao; na hata wakinywa kitu chochote cha kuua, hakitawadhuru kamwe; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona.”
Isa apaa mbinguni
(Luka 24:50-53; Matendo 1:9-11)
19Baada ya Bwana Isa kusema nao, alichukuliwa juu mbinguni na kuketi mkono wa kuume wa Mungu. 20Kisha wanafunzi wake wakatoka, wakahubiri kila mahali, naye Bwana Isa akatenda kazi pamoja nao na kulithibitisha neno lake kwa ishara zilizofuatana nalo.]

Iliyochaguliwa sasa

Marko 16: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia