Marko 3
3
Isa amponya mtu aliyepooza mkono
(Mathayo 12:9-14; Luka 6:6-11)
1Isa akaingia tena ndani ya sinagogi#3:1 Nyumba ya ibada na mafunzo., na kulikuwa na mtu aliyepooza mkono. 2Wakawa wanamwangalia waone kama atamponya huyo mtu siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki. 3Isa akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Njoo hapa mbele ya watu wote.”
4Kisha Isa akawauliza, “Je, ni lipi lililo halali siku ya Sabato: Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao wakanyamaza.
5Isa akawatazama kwa hasira watu waliomzunguka pande zote, akahuzunika sana kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukawa umeponywa kabisa! 6Kisha Mafarisayo wakatoka nje, nao wakaanza kufanya njama ya kumuua Isa wakishirikiana na Maherode#3:6 Wafuasi wa Mfalme Herode waliokubaliana na utawala wa Rumi..
Makundi ya watu wamfuata Isa
7Isa na wanafunzi wake wakaondoka huko, wakaenda baharini, nao umati mkubwa wa watu kutoka Galilaya wakamfuata. 8Waliposikia mambo yote aliyokuwa akiyafanya, makundi ya watu wakamjia kutoka Yudea, Yerusalemu, Idumaya, na ng’ambo ya Yordani, pamoja na wale wa maeneo ya Tiro na Sidoni. 9Kwa sababu ya umati mkubwa wa watu, aliwaambia wanafunzi wake watayarishe mashua ndogo kwa ajili yake, ili kuwazuia watu kumsonga. 10Kwa kuwa alikuwa amewaponya wagonjwa wengi, wale wenye magonjwa walikuwa wanasukumana ili wapate kumgusa. 11Kila mara pepo wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kupiga kelele wakisema, “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu#3:11 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili..” 12Lakini aliwaonya wasiwaambie wengine kumhusu.
Isa achagua mitume kumi na wawili
(Mathayo 10:1-4; Luka 6:12-16)
13Isa akapanda mlimani na kuwaita wale aliowataka, nao wakamjia. 14Akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume, ili wapate kuwa naye, na awatume kwenda kuhubiri 15na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu.
16Hawa ndio wale kumi na wawili aliowachagua:
Simoni (ambaye alimwita Petro);
17Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye (ambao aliwaita Boanerge, maana yake Wana wa Ngurumo);
18Andrea,
Filipo,
Bartholomayo,
Mathayo,
Tomaso,
Yakobo mwana wa Alfayo,
Thadayo,
Simoni Mkananayo#3:18 yaani Mzelote; Wazelote walikuwa kikundi cha Kiyahudi wenye imani kali waliompinga Kaisari na utawala wa Rumi.,
19na Yuda Iskariote aliyemsaliti Isa.
Isa na Beelzebuli
(Mathayo 12:22-32; Luka 11:14-23)
20Kisha Isa alipoingia ndani ya nyumba, umati wa watu wakakusanyika tena, kiasi kwamba yeye na wanafunzi wake hawakuweza kula chakula. 21Ndugu zake walipopata habari wakaja ili kumchukua kwa maana watu walikuwa wakisema, “Amerukwa na akili.”
22Walimu wa Torati walioteremka kutoka Yerusalemu walisema, “Amepagawa na Beelzebuli#3:22 kwa Kiyunani ni Beelzebubu, yaani mkuu wa pepo wachafu! Anatoa pepo wachafu kwa nguvu ya mkuu wa pepo wachafu!”
23Basi Isa akawaita na kuzungumza nao kwa mifano akasema: “Shetani awezaje kumtoa Shetani? 24Kama ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama. 25Nayo nyumba ikigawanyika dhidi yake yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama. 26Na kama Shetani akijipinga mwenyewe na awe amegawanyika, hawezi kusimama, bali mwisho wake umetimia. 27Hakuna mtu yeyote awezaye kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali yake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu. Ndipo ataweza kuteka nyara mali yake. 28Amin, nawaambia, watu wataweza kusamehewa dhambi na kufuru zao zote; 29lakini yeyote anayemkufuru Roho Mtakatifu wa Mungu hatasamehewa kamwe, atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.”
30Isa alisema hivi kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”
Mama yake na ndugu zake Isa
(Mathayo 12:46-50; Luka 8:19-21)
31Kisha wakaja ndugu zake Isa pamoja na mama yake. Wakiwa wamesimama nje, wakamtuma mtu kumwita. 32Umati wa watu walikuwa wameketi kumzunguka, nao wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.”
33Akawauliza, “Mama yangu na ndugu zangu ni nani?”
34Kisha akawatazama wale watu waliokuwa wameketi kumzunguka pande zote, akasema, “Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu. 35Mtu yeyote anayetenda mapenzi ya Mungu, huyo ndiye kaka yangu, na dada yangu, na mama yangu.”
Iliyochaguliwa sasa
Marko 3: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.