Marko 4
4
Mfano wa mpanzi
(Mathayo 13:1-9; Luka 8:1-8)
1Isa akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Palikuwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekusanyika kumzunguka, hata ikambidi Isa aingie kwenye mashua iliyokuwa baharini na kuketi humo, nao watu wote walikuwa ufuoni mwa bahari. 2Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, naye katika mafundisho yake akasema: 3“Sikilizeni! Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu 4Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila. 5Nyingine zilianguka kwenye mwamba usio na udongo mwingi. Ziliota haraka kwa kuwa udongo ulikuwa kidogo. 6Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina. 7Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba ikakua, ikaisonga hiyo mimea, hivyo haikutoa mazao. 8Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri, zikaota vizuri na kukua, zikatoa mazao, moja mara thelathini, nyingine mara sitini, na nyingine mara mia moja.”
9Kisha Isa akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”
Sababu ya kufundisha kwa mifano
(Mathayo 13:10-17; Luka 8:9-10)
10Alipokuwa peke yake, watu waliokuwa naye pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili wakamuuliza kuhusu mifano yake. 11Naye akawaambia, “Ninyi mmepewa siri ya ufalme wa Mungu. Lakini kwa wale walio nje, kila kitu husemwa kwa mifano, 12ili,
“ ‘kuona waone lakini wasitambue,
na kusikia wasikie lakini wasielewe;
wasije wakageuka na kusamehewa!’#4:12 Isaya 6:9, 10”
Maelezo ya mfano wa mbegu
(Mathayo 13:18-23; Luka 8:11-15)
13Kisha Isa akawauliza, “Hamwelewi maana ya mfano huu? Basi mtaelewaje mifano mingine? 14Yule mpanzi hupanda neno. 15Hawa ndio wale walio kando ya njia ambako neno lilipandwa. Walisikiapo neno, mara Shetani huja na kulinyakua lile neno lililopandwa ndani yao. 16Nazo zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye miamba, ni wale wanaolisikia neno, na mara hulipokea kwa furaha. 17Lakini kwa kuwa hawana mizizi, wao hudumu kwa muda mfupi tu. Kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, mara wao huiacha imani. 18Lakini wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye miiba, hulisikia lile neno; 19lakini masumbufu ya maisha haya, na udanganyifu wa mali na tamaa ya mambo mengine huja na kulisonga lile neno na kulifanya lisizae. 20Wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri, hulisikia lile neno, wakalipokea na kuzaa mazao. Wao huzaa mara thelathini, au mara sitini, au mara mia ya mbegu iliyopandwa.”
Mfano wa taa
(Luka 8:16-18)
21Akawaambia, “Je, taa huwashwa na kufunikwa chini ya kikapu au mvunguni mwa kitanda? Je, haiwashwi na kuwekwa juu ya kinara chake? 22Kwa kuwa hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna jambo lolote la siri ambalo halitaletwa nuruni. 23Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”
24Naye akawaambia, “Kuweni waangalifu na yale mnayosikia. Kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa ninyi, hata na zaidi. 25Kwa maana kila mtu aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.”
Mfano wa mbegu inayoota
26Pia akawaambia, “Ufalme wa Mungu unafanana na mtu apandaye mbegu shambani. 27Baada yake kuzipanda, usiku na mchana, akiwa amelala au ameamka, mbegu huota na kukua pasipo yeye kujua ikuavyo. 28Udongo huifanya iote kuwa mche, halafu suke, kisha nafaka kamili kwenye suke. 29Mara nafaka inapokuwa imekomaa, mkulima huenda shambani na mundu kuvuna, maana mavuno yamekuwa tayari.”
Mfano wa punje ya haradali
(Mathayo 13:31-32; Luka 13:18-19)
30Akawaambia tena, “Tuufananishe ufalme wa Mungu na nini? Au tutumie mfano gani ili kuueleza? 31Ni kama punje ya haradali, ambayo ni mbegu ndogo sana kuliko mbegu zote zinazopandwa ardhini. 32Lakini ikipandwa, hukua ikawa mmea mkubwa kuliko yote katika bustani, ikawa na matawi makubwa hata ndege wa angani wanaweza kujenga viota kwenye kivuli chake.”
33Kwa mifano mingine mingi kama hii Isa alinena nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulielewa. 34Hakusema nao neno lolote pasipo mfano. Lakini alipokuwa na wanafunzi wake, aliwafafanulia kila kitu.
Isa atuliza dhoruba
(Mathayo 8:23-27; Luka 8:22-25)
35Ilipokaribia jioni ya siku hiyo, Isa akawaambia wanafunzi wake, “Tuvukeni hadi ng’ambo ya ziwa.” 36Wakaacha umati wa watu, na wakamchukua vile alivyokuwa kwenye mashua. Palikuwa pia na mashua zingine nyingi pamoja naye. 37Kukawa na dhoruba kali, nayo mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikawa karibu kujaa maji. 38Isa alikuwa katika shetri, akiwa analala juu ya mto. Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kama tunazama?”
39Akaamka, akaukemea ule upepo, akayaambia yale mawimbi, “Uwe kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari kabisa.
40Isa akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa hivyo? Je, bado hamna imani?”
41Nao wakawa wameogopa sana, wakaulizana, “Ni nani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!”
Iliyochaguliwa sasa
Marko 4: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.