Marko 8:1-13
Marko 8:1-13 NENO
Katika siku hizo, umati mkubwa wa watu walikusanyika tena. Kwa kuwa walikuwa hawana chakula, Isa akawaita wanafunzi wake akawaambia, “Ninahurumia umati huu wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula. Nikiwaaga waende nyumbani bila kula, watazimia njiani kwa sababu baadhi yao wametoka mbali.” Wanafunzi wake wakamjibu, “Lakini hapa nyikani tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha?” Isa akawauliza, “Mna mikate mingapi?” Wakajibu, “Tuna mikate saba.” Akawaambia watu waketi chini. Akaichukua ile mikate saba na kushukuru, baadaye akaimega na kuwapa wanafunzi wake ili wawagawie watu. Wanafunzi wake wakafanya hivyo. Walikuwa pia na visamaki vichache, Isa akavibariki, akawaamuru wanafunzi wake wawagawie watu. Wale watu walikula na kutosheka. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba. Watu waliokula walikuwa wapata elfu nne. Baada ya kuwaaga, aliingia kwenye mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda sehemu za Dalmanutha. Mafarisayo wakaja, wakaanza kumhoji Isa. Ili kumtega, wakamwomba awaoneshe ishara kutoka mbinguni. Akahuzunika moyoni, akawaambia, “Kwa nini kizazi hiki kinataka ishara? Amin nawaambieni, hakitapewa ishara yoyote.” Kisha akawaacha, akarudi kwenye mashua, akavuka hadi ng’ambo.