Marko 8:1-13
Marko 8:1-13 SRUV
Katika siku zile, kwa vile ulivyokuwa mkuu tena ule mkutano, nao wamekosa kitu cha kula, akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Nawahurumia mkutano kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula; nami nikiwaaga waende zao nyumbani kwao wakiwa na njaa, watazimia njiani; na baadhi yao wametoka mbali. Wanafunzi wake wakamjibu, Je! Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani? Akawauliza, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawaandalie; wakawaandalia mkutano. Walikuwa na visamaki vichache; akavibariki, akasema wawagawie na hivyo pia. Wakala, wakashiba, wakakusanya mabaki ya vipande vya mikate vikapu saba. Na watu waliokula walikuwa elfu nne. Akawaaga. Mara akapanda katika mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda pande za Dalmanutha. Wakatokea Mafarisayo, wakaanza kuhojiana naye; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni; wakimjaribu. Akapiga kite rohoni mwake, akasema, Mbona kizazi hiki chatafuta ishara? Amin, nawaambieni, Hakitapewa ishara kizazi hiki. Akawaacha, akapanda tena katika mashua, akaenda zake hadi ng'ambo.