Wafilipi 4
4
Mausia
1Kwa hiyo, ndugu zangu, ninaowapenda na ambao ninawaonea shauku, ninyi mlio furaha yangu na taji langu, hivi ndivyo iwapasavyo kusimama imara katika Bwana Isa, ninyi wapendwa wangu.
2Nawasihi Euodia na Sintike wawe na nia moja katika Bwana Isa. 3Naam, nakusihi wewe pia, mwenzangu mwaminifu, uwasaidie hawa wanawake, kwa sababu walijitaabisha katika kazi ya Injili pamoja nami bega kwa bega, wakiwa pamoja na Klementi na watendakazi wenzangu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima.
4Furahini katika Bwana Isa siku zote, tena nasema furahini! 5Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana Isa yu karibu. 6Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Al-Masihi Isa.
8Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo. 9Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.
Shukrani kwa matoleo yao
10Nina furaha kubwa katika Bwana Isa kwamba hatimaye mmeanza upya kushughulika tena na maisha yangu. Kweli mmekuwa mkinifikiria lakini mlikuwa hamjapata nafasi ya kufanya hivyo. 11Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
14Lakini, mlifanya vyema kushiriki nami katika taabu zangu. 15Zaidi ya hayo, ninyi Wafilipi mnajua kwamba siku za kwanza nilipoanza kuhubiri Injili, nilipoondoka Makedonia, hakuna kundi lingine la waumini lililoshiriki nami katika masuala ya kutoa na kupokea isipokuwa ninyi. 16Kwa maana hata nilipokuwa huko Thesalonike, mliniletea msaada kwa ajili ya mahitaji yangu zaidi ya mara moja. 17Si kwamba natafuta sana yale matoleo, bali natafuta sana ile faida itakayozidi sana kwa upande wenu. 18Nimelipwa kikamilifu hata na zaidi; nimetoshelezwa kabisa sasa, kwa kuwa nimepokea kutoka kwa Epafrodito vile vitu mlivyonitumia, sadaka yenye harufu nzuri, dhabihu inayokubalika na ya kumpendeza Mungu. 19Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Al-Masihi Isa.
20Mungu wetu aliye Baba#4:20 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yetu apewe utukufu milele na milele. Amen.
Salamu za mwisho
21Msalimuni kila mtakatifu katika Al-Masihi Isa.
Ndugu walio pamoja nami wanawasalimu.
22Watakatifu wote wanawasalimu, hasa wale watu wa nyumbani mwa Kaisari.
23Neema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi iwe pamoja na roho zenu. Amen.
Iliyochaguliwa sasa
Wafilipi 4: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.