Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 11

11
1Mwenyezi Mungu huchukia sana mizani za udanganyifu,
bali vipimo sahihi ni furaha yake.
2Kiburi kinapokuja, ndipo huja aibu,
bali unyenyekevu huja na hekima.
3Uadilifu wa wenye haki huwaongoza,
bali wasio waaminifu huangamizwa na hila yao.
4Utajiri haufaidi kitu katika siku ya ghadhabu,
bali haki huokoa kutoka mautini.
5Haki ya wasio na lawama, huwatengenezea njia iliyo nyofu,
bali waovu huangushwa kwa uovu wao wenyewe.
6Haki ya wanyofu huwaokoa,
bali wasio waaminifu hunaswa na tamaa mbaya.
7Matumaini yaliyo katika wanadamu hufa pamoja nao;
ahadi zote za uwezo wao hubatilika.
8Mtu mwenye haki huokolewa kutoka taabu,
naye mtu mwovu huingia humo badala yake.
9Kwa kinywa chake mtu asiyemwamini Mungu
humwangamiza jirani yake,
bali kwa maarifa mwenye haki huokolewa.
10Mwenye haki anapofanikiwa, mji hufurahi;
mwovu anapoangamia, kuna shangwe za furaha.
11Kutokana na baraka ya mtu mnyofu mji hukwezwa,
bali kwa kinywa cha mwovu mji huharibiwa.
12Mtu asiye na akili humdharau jirani yake,
bali mtu mwenye ufahamu huuzuia ulimi wake.
13Masengenyo husaliti uaminifu,
bali mtu mwaminifu hutunza siri.
14Pasipo ushauri wa hekima taifa huanguka,
bali washauri wengi hufanya ushindi uwe wa hakika.
15Yeye amdhaminiye mgeni hakika atateseka,
bali yeyote akataaye kuunga mkono dhamana ni salama.
16Mwanamke mwenye moyo wa huruma hupata heshima,
bali wanaume wakorofi hupata mali tu.
17Mwenye huruma hujinufaisha mwenyewe,
bali mkatili hujiletea taabu mwenyewe.
18Mtu mwovu hupata ujira wa udanganyifu,
bali yeye apandaye haki huvuna tuzo ya uhakika.
19Mtu mwenye haki kweli kweli hupata uzima,
bali yeye afuatiliaye ubaya huendea kifo chake.
20Mwenyezi Mungu huwachukia sana watu wenye moyo wa upotovu,
bali hupendezwa na wale ambao njia zao hazina lawama.
21Uwe na hakika na hili: Waovu hawataepuka kuadhibiwa,
bali wenye haki watakuwa huru.
22Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe
ndivyo alivyo mwanamke mzuri ambaye hana busara.
23Shauku ya mwenye haki huishia tu kwenye mema,
bali tumaini la mwovu huishia tu kwenye ghadhabu.
24Kuna mtu atoaye kwa ukarimu, hata hivyo hupata zaidi,
mwingine huzuia, lakini huwa maskini.
25Mtu mkarimu atastawi;
yeye awaburudishaye wengine
ataburudishwa mwenyewe.
26Watu humlaani mtu awanyimae watu nafaka,
bali baraka itamkalia kichwani kama taji
yeye aliye radhi kuiuza.
27Yeye atafutaye mema hupata ukarimu,
bali ubaya huja kwake yeye autafutaye.
28Yeyote ategemeaye utajiri wake ataanguka,
bali mwenye haki atastawi kama jani bichi.
29Yeye aletaye taabu kwa jamaa yake atarithi tu upepo,
naye mpumbavu atakuwa mtumishi wa wenye hekima.
30Tunda la mwenye haki ni mti wa uzima,
naye mwenye hekima huokoa maisha.
31Kama wenye haki watapokea ujira wao duniani,
si zaidi sana mtu asiyemcha Mungu,
na mwenye dhambi?

Iliyochaguliwa sasa

Mithali 11: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia