Mithali 10
10
Mithali za Sulemani
1Mithali za Sulemani:
Mwana mwenye hekima
huleta furaha kwa baba yake,
lakini mwana mpumbavu
huleta huzuni kwa mama yake.
2Hazina zilizopatikana kwa njia mbaya hazifai,
lakini uadilifu huokoa kutoka mautini.
3Mwenyezi Mungu hawaachi waadilifu kukaa njaa,
lakini hupinga tamaa ya mtu mwovu.
4Mikono mivivu hufanya mtu kuwa maskini
lakini mikono yenye bidii huleta utajiri.
5Yeye akusanyaye mazao wakati wa kiangazi
ni mwana mwenye hekima,
lakini yeye alalaye wakati wa mavuno
ni mwana mwenye kuaibisha.
6Baraka huwa taji kichwani mwa mwenye haki,
lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.
7Kumbukumbu ya mwenye haki itakuwa baraka,
lakini jina la mwovu litaoza.
8Mwenye hekima moyoni hupokea maagizo,
lakini mpumbavu apayukaye huangamia.
9Mtu mwadilifu hutembea salama,
lakini mtu aendaye katika njia zilizopotoka atagunduliwa.
10Yeye akonyezaye kwa nia mbaya husababisha huzuni,
naye mpumbavu apayukaye huangamia.
11Kinywa cha mwenye haki ni chemchemi ya uzima,
lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.
12Chuki huchochea faraka,
lakini upendo husitiri mabaya yote.
13Hekima hupatikana katika midomo ya wenye kupambanua,
lakini fimbo ni kwa ajili ya mgongo wake asiye na ufahamu.
14Wenye hekima huhifadhi maarifa,
bali kinywa cha mpumbavu hualika maangamizi.
15Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome,
bali ufukara ni maangamizi ya maskini.
16Ujira wa wenye haki huwaletea uzima,
lakini mapato ya waovu ni dhambi na mauti.
17Anayekubali kuadibishwa yuko katika njia ya uzima,
lakini yeyote anayepuuza maonyo hupotosha wengine.
18Yeye afichaye chuki yake ana midomo ya uongo,
na yeyote anayeeneza uchonganishi ni mpumbavu.
19Dhambi haiondolewi kwa maneno mengi,
bali wenye busara huzuia ulimi wao.
20Ulimi wa mwenye haki ni fedha iliyo bora,
bali moyo wa mwovu una thamani ndogo.
21Midomo ya mwenye haki hulisha wengi,
lakini wapumbavu hufa kwa kukosa ufahamu.
22Baraka ya Mwenyezi Mungu hutajirisha,
wala haichanganyi na huzuni.
23Mpumbavu hufurahia hila,
lakini mtu mwenye ufahamu hupendezwa na hekima.
24Kile anachoogopa mwovu ndicho kitakachompata;
kile anachoonea shauku mwenye haki atapewa.
25Tufani inapopita, waovu hutoweka,
lakini wenye haki husimama imara milele.
26Kama siki ilivyo kwa meno na moshi kwa macho,
ndivyo alivyo mvivu kwa wale waliomtuma.
27Kumcha Mwenyezi Mungu huongeza urefu wa maisha,
lakini miaka ya mwovu inafupishwa.
28Tarajio la mwenye haki ni furaha,
bali matumaini ya mwovu huwa si kitu.
29Njia ya Mwenyezi Mungu ni kimbilio kwa wenye haki,
lakini ni maangamizi ya wale watendao mabaya.
30Kamwe wenye haki hawataondolewa,
bali waovu hawatasalia katika nchi.
31Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima,
bali ulimi wa upotovu utakatwa.
32Midomo ya wenye haki hujua kile chenye kibali,
bali kinywa cha mwovu hujua kile kilichopotoka tu.
Iliyochaguliwa sasa
Mithali 10: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.