Mithali 13
13
Mema ya muda mfupi na yale ya kudumu
1Mwana mwenye hekima husikia mafundisho ya babaye,
bali mwenye dharau hasikilizi maonyo.
2Kutoka tunda la midomo yake, mtu hufurahia mambo mema,
bali wasio waaminifu wanatamani sana jeuri.
3Yeye alindaye midomo yake hulinda nafsi yake,
bali yeye asemaye kwa haraka ataangamia.
4Mvivu hutamani sana na hapati kitu,
bali nafsi ya mwenye bidii
hutoshelezwa kikamilifu.
5Mwenye haki huchukia uongo,
bali waovu huleta aibu na fedheha.
6Haki humlinda mtu mwadilifu,
bali uovu humwangusha mwenye dhambi.
7Mtu mmoja hujifanya tajiri, kumbe hana chochote;
mwingine hujifanya maskini, kumbe ana utajiri mwingi.
8Utajiri wa mtu unaweza kukomboa maisha yake,
bali mtu maskini hasikii kitisho.
9Nuru ya mwenye haki hung’aa sana,
bali taa ya mwovu itazimwa.
10Kiburi huzalisha magomvi tu,
bali hekima hupatikana kwa wale wanaozingatia ushauri.
11Fedha isiyo ya halali hupungua,
bali yeye akusanyaye fedha kidogo kidogo huongezeka.
12Kilichotarajiwa kikikawia kuja moyo huugua,
bali tumaini lililotimizwa ni mti wa uzima.
13Yeye anayedharau mafundisho anajiletea maangamizi,
bali yeye anayeheshimu agizo hupewa tuzo.
14Mafundisho ya mwenye busara ni chemchemi ya uzima,
ili kumwepusha mtu na mitego ya mauti.
15Ufahamu mzuri hupata upendeleo,
bali njia ya asiye mwaminifu ni ngumu.
16Kila mwenye busara hutenda kwa maarifa,
bali mpumbavu hudhihirisha upumbavu wake.
17Mjumbe mwovu huanguka kwenye taabu,
bali mjumbe mwaminifu huleta uponyaji.
18Yeye anayedharau maonyo hupata umaskini na aibu,
bali yeye anayekubali maonyo huheshimiwa.
19Tarajio lililotimizwa ni tamu kwa nafsi,
bali wapumbavu huchukia sana kuacha ubaya.
20Yeye atembeaye na mwenye hekima atapata hekima,
bali rafiki wa mpumbavu hupata madhara.
21Balaa humwandama mtenda dhambi,
bali mafanikio ni thawabu kwa mwenye haki.
22Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi,
bali mali ya wenye dhambi imehifadhiwa
kwa ajili ya wenye haki.
23Shamba la mtu maskini laweza kuzalisha chakula kingi,
bali dhuluma hukifutilia mbali.
24Yeye asiyetumia fimbo yake hampendi mwanawe,
bali yeye ampendaye
huwa mwangalifu kumwadibisha.
25Mwenye haki hula hadi akaridhisha moyo wake,
bali tumbo la mwovu hutaabika kwa njaa.
Iliyochaguliwa sasa
Mithali 13: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.