Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 14

14
1Mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake,
bali mpumbavu huibomoa nyumba yake
kwa mikono yake mwenyewe.
2Yeye ambaye njia zake ni nyofu humcha Mwenyezi Mungu,
bali yeye ambaye njia zake zimepotoka humdharau Mungu.
3Mazungumzo ya mpumbavu huleta fimbo mgongoni mwake,
bali mwenye hekima hulindwa na maneno ya midomo yake.
4Pale ambapo hakuna mafahali, hori ni tupu,
bali kutokana na nguvu za fahali huja mavuno mengi.
5Shahidi mwaminifu hadanganyi,
bali shahidi wa uongo humimina uongo.
6Mwenye mzaha huitafuta hekima na haipati,
bali maarifa huja kwa urahisi kwa anayepambanua.
7Kaa mbali na mtu mpumbavu,
kwa maana hutapata maarifa katika midomo yake.
8Hekima ya mwenye busara ni kufikiria njia zake,
bali upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu.
9Wapumbavu hudhihaki kujirekebisha kutoka dhambi,
bali wema hupatikana miongoni mwa wanyofu.
10Kila moyo hujua uchungu wake wenyewe,
wala hakuna yeyote awezaye kushiriki furaha yake.
11Nyumba ya mwovu itaangamizwa,
bali hema la mnyofu litastawi.
12Iko njia ionekanayo kuwa sawa kwa mtu,
bali mwisho wake huelekeza mautini.
13Hata katika kicheko moyo unaweza kuuma,
nayo furaha yaweza kuishia katika majonzi.
14Wasio na imani watapatilizwa kikamilifu kwa ajili ya njia zao,
naye mtu mwema atapewa thawabu kwa ajili ya njia yake.
15Mtu mjinga huamini kila kitu,
bali mwenye busara hufikiria hatua zake.
16Mtu mwenye hekima humcha Mwenyezi Mungu na kuepuka mabaya,
bali mpumbavu hukasirika kwa hamaki na uzembe.
17Mtu anayekasirika kwa haraka hufanya mambo ya upumbavu,
naye mtu wa hila huchukiwa.
18Mjinga hurithi upumbavu,
bali wenye busara huvikwa maarifa kichwani kama taji.
19Wapotovu watasujudu mbele ya watu wema,
nao waovu kwenye malango ya wenye haki.
20Maskini huepukwa hata na majirani zao,
bali matajiri wana rafiki wengi.
21Yeye anayemdharau jirani yake hutenda dhambi,
bali amebarikiwa yeye aliye na huruma kwa mhitaji.
22Je, wale wanaopanga ubaya hawapotoki?
Bali wale wanaopanga kilicho chema
hupata upendo na uaminifu.
23Kazi zote zinazofanywa kwa bidii huleta faida,
bali mazungumzo matupu huelekea umaskini tu.
24Utajiri wa wenye hekima ni taji lao,
bali upumbavu wa wapumbavu huzaa upumbavu.
25Shahidi wa kweli huokoa maisha,
bali shahidi wa uongo ni mdanganyifu.
26Yeye amchaye Mwenyezi Mungu ana ngome salama,
na kwa watoto wake itakuwa kimbilio.
27Kumcha Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya uzima,
ili kumwepusha mtu na mitego ya mauti.
28Wingi wa watu ni utukufu wa mfalme,
bali pasipo watu mkuu huangamia.
29Mtu mwenye subira ana ufahamu mwingi,
bali anayekasirika haraka huonesha upumbavu.
30Moyo wenye amani huupa mwili uzima,
bali wivu huozesha mifupa.
31Yeye anayemdhulumu maskini humdharau Muumba wao,
bali yeyote anayemhurumia mhitaji humheshimu Mungu.
32Waovu huangamizwa kwa matendo yao maovu,
bali hata katika kifo wenye haki hupata kimbilio.
33Hekima hukaa katika moyo wa mwenye ufahamu
bali haijulikani miongoni mwa wapumbavu.
34Haki huinua taifa,
bali dhambi ni aibu kwa watu wote.
35Mfalme hupendezwa na mtumishi mwenye hekima,
bali ghadhabu yake humwangukia
mtumishi mwenye kuaibisha.

Iliyochaguliwa sasa

Mithali 14: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia