Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 17

17
1Afadhali kula ukoko mkavu ukiwa na amani na utulivu
kuliko kukaa kwenye nyumba ya karamu kukiwa na magomvi.
2Mtumishi mwenye hekima atamtawala mwana aaibishaye,
naye atashirikiana katika urithi kama mmoja wa hao ndugu.
3Kalibu husafisha fedha na tanuru husafisha dhahabu,
bali Mwenyezi Mungu huujaribu moyo.
4Mtu mwovu husikiliza midomo mibaya;
mwongo husikiliza kwa makini ulimi wa madhara.
5Yeye anaye mdhihaki maskini huonesha dharau kwa Muumba wake;
yeyote afurahiaye maafa hataepuka kuadhibiwa.
6Wana wa wana ni taji la wazee,
nao wazazi ni fahari ya watoto wao.
7Midomo yenye uwezo wa ushawishi
haimfai mpumbavu:
je, ni mibaya kiasi gani zaidi
midomo ya uongo kwa mtawala!
8Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho;
kokote kigeukiapo, hufanikiwa.
9Yeye anayesamehe kosa hudumisha upendo,
bali yeyote arudiaye jambo huwatenganisha rafiki wa karibu.
10Karipio humwingia sana mtu mwenye kutambua
kuliko mapigo mia kwa mpumbavu.
11Mwovu hupenda kuasi tu;
mjumbe asiye na huruma atatumwa dhidi yake.
12Ni afadhali ukutane na dubu aliyenyang’anywa watoto wake,
kuliko mpumbavu katika upumbavu wake.
13Ikiwa mtu atalipa baya kwa jema,
kamwe ubaya hautaondoka katika nyumba yake.
14Kuanzisha ugomvi ni kama kutoboa bwawa la maji;
kwa hiyo acha jambo hilo kabla mabishano hayajaanza.
15Yeye asemaye kuwa asiye na haki ana haki,
naye asemaye kuwa mwenye haki hana haki:
Mwenyezi Mungu huwachukia sana wote wawili.
16Fedha ina faida gani mikononi mwa mpumbavu,
wakati yeye hana haja ya kupata hekima?
17Rafiki hupenda wakati wote
naye ndugu amezaliwa kwa ajili ya wakati wa shida.
18Mtu mjinga huutoa mkono ili kuweka rehani,
naye huweka dhamana kwa jirani yake.
19Yeye apendaye ugomvi apenda dhambi;
naye ainuaye sana lango lake hutafuta uharibifu.
20Mtu mwenye moyo mpotovu hawezi kufanikiwa;
naye ambaye ulimi wake ni mdanganyifu huanguka kwenye taabu.
21Kuwa na mwana mpumbavu huleta huzuni;
hakuna furaha kwa baba wa mpumbavu.
22Moyo wenye furaha ni dawa nzuri,
bali roho iliyopondeka hukausha mifupa.
23Mtu mwovu hukubali rushwa kwa siri
ili kupotosha njia ya haki.
24Mtu wa ufahamu huitazama hekima,
lakini macho ya mpumbavu huhangaika
hadi kwenye miisho ya dunia.
25Mwana mpumbavu huleta huzuni kwa baba yake
na uchungu kwa yeye aliyemzaa.
26Si vizuri kumwadhibu mtu asiye na hatia,
au kuwapiga sana maafisa kwa ajili ya uadilifu wao.
27Mtu mwenye maarifa hutumia maneno kwa kujizuia,
naye mtu mwenye ufahamu ana moyo wa utulivu.
28Hata mtu mpumbavu hudhaniwa kuwa na hekima akinyamaza,
na mwenye ufahamu akiuzuia ulimi wake.

Iliyochaguliwa sasa

Mithali 17: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia