Zaburi 1:1-6
Zaburi 1:1-6 NENO
Heri mtu yule ambaye haendi katika shauri la watu waovu, wala hasimami katika njia ya wenye dhambi, au kuketi katika baraza la wenye mizaha. Bali huifurahia Torati ya Mwenyezi Mungu, naye huitafakari hiyo Torati usiku na mchana. Mtu huyo ni kama mti uliopandwa kando ya vijito vya maji, ambao huzaa matunda kwa majira yake na majani yake hayanyauki. Lolote afanyalo hufanikiwa. Sivyo walivyo waovu! Wao ni kama makapi yanayopeperushwa na upepo. Kwa hiyo waovu hawatastahimili hukumu, wala wenye dhambi katika kusanyiko la wenye haki. Kwa maana Mwenyezi Mungu huziangalia njia za mwenye haki, bali njia za waovu zitaangamia.