Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 33:1-12

Zaburi 33:1-12 NEN

Mwimbieni BWANA kwa furaha, enyi wenye haki; kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. Msifuni BWANA kwa kinubi, mwimbieni sifa kwa zeze la nyuzi kumi. Mwimbieni wimbo mpya; pigeni kwa ustadi, na mpaze sauti za shangwe. Maana neno la BWANA ni haki na kweli, ni mwaminifu kwa yote atendayo. BWANA hupenda uadilifu na haki; dunia imejaa upendo wake usiokoma. Kwa neno la BWANA mbingu ziliumbwa, jeshi lao la angani kwa pumzi ya kinywa chake. Ameyakusanya maji ya bahari kama kwenye chungu; vilindi vya bahari ameviweka katika ghala. Dunia yote na imwogope BWANA, watu wote wa dunia wamche. Kwa maana Mungu alisema, na ikawa, aliamuru na ikasimama imara. BWANA huzuia mipango ya mataifa, hupinga makusudi ya mataifa. Lakini mipango ya BWANA inasimama imara milele, makusudi ya moyo wake kwa vizazi vyote. Heri taifa ambalo BWANA ni Mungu wao, watu ambao aliwachagua kuwa urithi wake.