Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 35:19-28

Zaburi 35:19-28 NEN

Usiwaache wale wanaonisimanga, wale ambao ni adui zangu bila sababu; usiwaache wale ambao ni adui zangu bila sababu wakonyeze jicho kwa hila. Hawazungumzi kwa amani, bali wanatunga mashtaka ya uongo dhidi ya wale wanaoishi kwa utulivu katika nchi. Hunifumbulia vinywa vyao wakisema, “Aha! Aha! Kwa macho yetu wenyewe tumeliona.” Ee BWANA, umeona hili, usiwe kimya. Usiwe mbali nami, Ee BWANA. Amka, inuka unitetee! Unipiganie Mungu wangu na Bwana wangu. Nihukumu kwa haki yako, Ee BWANA Mungu wangu, sawasawa na haki yako; usiwaache wakusimange. Usiwaache wafikiri, “Aha, hili ndilo tulilotaka!” Au waseme, “Tumemmeza.” Wote wanaofurahia dhiki yangu waaibishwe na wachanganyikiwe; hao wanaojiinua dhidi yangu wavikwe aibu na dharau. Wale wanaofurahia hukumu yangu ya haki wapige kelele za shangwe na furaha; hebu waseme siku zote, “BWANA atukuzwe, ambaye amefurahia mafanikio ya mtumishi wake.” Ulimi wangu utanena haki yako na sifa zako mchana kutwa.