Zaburi 37
37
Zaburi 37#37 Zaburi hii imetungwa kila beti likianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.
Mwisho wa mwovu na urithi wa mwenye haki
Zaburi ya Daudi.
1Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu,
wala usiwaonee wivu watendao mabaya,
2kwa maana watanyauka upesi kama majani,
watakufa upesi kama mimea ya kijani.
3Mtumaini Mwenyezi Mungu na utende yaliyo mema.
Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama.
4Jifurahishe katika Mwenyezi Mungu
naye atakupa haja za moyo wako.
5Mkabidhi Mwenyezi Mungu njia yako,
mtumaini yeye, naye atatenda hili:
6Yeye atafanya haki yako ing’ae kama mapambazuko,
na hukumu ya shauri lako kama jua la adhuhuri.
7Tulia mbele za Mwenyezi Mungu
na umngojee kwa uvumilivu;
usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao,
wanapotekeleza mipango yao miovu.
8Epuka hasira na uache ghadhabu;
usihangaike: itakuongoza tu kutenda uovu.
9Kwa maana waovu watakatiliwa mbali,
bali wale wanaomtumaini Mwenyezi Mungu watairithi nchi.
10Bado kitambo kidogo, nao waovu hawataonekana,
ingawa utawatafuta, hawataonekana.
11Bali wanyenyekevu watairithi nchi
na wafurahie amani tele.
12Waovu hula njama dhidi ya wenye haki
na kuwasagia meno,
13bali Bwana huwacheka waovu,
kwa sababu anajua siku yao inakuja.
14Waovu hufuta upanga
na kupinda upinde,
ili wawaangushe maskini na wahitaji,
kuwaua wale ambao njia zao ni nyofu.
15Lakini panga zao zitachoma mioyo yao wenyewe,
na pinde zao zitavunjwa.
16Bora kidogo walicho nacho wenye haki
kuliko wingi wa mali ya waovu wengi;
17kwa maana nguvu za waovu zitavunjwa,
lakini Mwenyezi Mungu humtegemeza mwenye haki.
18Mwenyezi Mungu anazifahamu siku za wanyofu,
na urithi wao utadumu milele.
19Siku za maafa hawatanyauka,
siku za njaa watafurahia wingi wa vitu.
20Lakini waovu wataangamia:
Adui za Mwenyezi Mungu watakuwa
kama uzuri wa mashamba,
watatoweka,
watatoweka kama moshi.
21Waovu hukopa na hawalipi,
bali wenye haki hutoa kwa ukarimu.
22Wale wanaobarikiwa na Mwenyezi Mungu watairithi nchi,
bali wale anaowalaani watakatiliwa mbali.
23Kama Mwenyezi Mungu akipendezwa na njia ya mtu,
yeye huimarisha hatua zake,
24ajapojikwaa, hataanguka,
kwa maana Mwenyezi Mungu
humtegemeza kwa mkono wake.
25Nilikuwa kijana na sasa ni mzee,
lakini sijaona kamwe wenye haki wameachwa
au watoto wao wakiombaomba chakula.
26Wakati wote ni wakarimu na hukopesha bila masharti.
Watoto wao watabarikiwa.
27Acha ubaya na utende wema,
nawe utaishi katika nchi milele.
28Kwa kuwa Mwenyezi Mungu huwapenda wenye haki
naye hatawaacha waaminifu wake.
Watalindwa milele,
lakini uzao wa waovu utakatiliwa mbali.
29Wenye haki watairithi nchi,
na kuishi humo milele.
30Kinywa cha mwenye haki hutamka hekima,
nao ulimi wake huzungumza lililo haki.
31Torati ya Mungu wake imo moyoni mwake;
nyayo zake hazitelezi.
32Watu waovu huvizia wenye haki,
wakitafuta kuwaua;
33lakini Mwenyezi Mungu hatawaacha mikononi mwao
wala hatawaacha wahukumiwe
kuwa wakosa wanaposhtakiwa.
34Mngojee Mwenyezi Mungu,
na uishike njia yake.
Naye atakutukuza uirithi nchi,
waovu watakapokatiliwa mbali,
utaliona hilo.
35Nimemwona mtu mwovu na mkatili akistawi
kama mwerezi wa Lebanoni,
36lakini alitoweka upesi na hakuonekana,
ingawa nilimtafuta, hakupatikana.
37Watafakari watu wasio na hatia,
wachunguze watu wakamilifu,
kuna mafanikio kwa mtu apendaye amani.
38Lakini watenda dhambi wote wataangamizwa,
mafanikio yao yatakatiliwa mbali.
39Wokovu wa wenye haki hutoka kwa Mwenyezi Mungu,
yeye ni ngome yao wakati wa shida.
40Mwenyezi Mungu huwasaidia na kuwaokoa,
huwaokoa kutoka kwa waovu na kuwahifadhi,
kwa maana wanamkimbilia.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 37: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.