Zaburi 45:9-17
Zaburi 45:9-17 NENO
Binti za wafalme ni miongoni mwa wanawake wako waheshimiwa; kuume kwako yupo bibi arusi malkia aliyevaa dhahabu ya Ofiri. Sikiliza, ewe binti, fikiri na utege sikio: Sahau watu wako na nyumba ya baba yako. Mfalme ameshangazwa na uzuri wako; mheshimu, kwa kuwa yeye ni bwana wako. Binti Tiro atakuletea zawadi, watu wenye utajiri watatafuta upendeleo wako. Ufahari wote una binti mfalme katika chumba chake; vazi lake limefumwa kwa nyuzi za dhahabu. Anaongozwa kwa mfalme, akiwa amevalia mavazi yaliyotariziwa, mabikira wenzake wanamfuata na wanaletwa kwako. Wanaingizwa ndani kwa shangwe na furaha, na kuingia katika jumba la mfalme. Wana wenu watachukua nafasi za baba zenu, mtawafanya wakuu katika nchi yote. Nitadumisha kumbukumbu lako katika vizazi vyote, kwa hiyo mataifa watakusifu milele na milele.