Zaburi 63:1-11
Zaburi 63:1-11 NEN
Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu, nakutafuta kwa moyo wote; nafsi yangu inakuonea kiu, mwili wangu unakuonea wewe shauku, katika nchi kame na iliyochoka mahali ambapo hapana maji. Nimekuona katika mahali patakatifu na kuuona uwezo wako na utukufu wako. Kwa sababu upendo wako ni bora kuliko uhai, midomo yangu itakuadhimisha. Nitakusifu siku zote za maisha yangu, na kwa jina lako nitainua mikono yangu. Nafsi yangu itatoshelezwa kama kwa wingi wa vyakula; kwa midomo iimbayo kinywa changu kitakusifu wewe. Kitandani mwangu ninakukumbuka wewe, ninawaza juu yako makesha yote ya usiku. Kwa sababu wewe ndiwe msaada wangu, chini ya uvuli wa mbawa zako naimba. Nafsi yangu inaambatana nawe, mkono wako wa kuume hunishika. Wale wanaotafuta uhai wangu wataharibiwa, watakwenda chini kwenye vilindi vya dunia. Watatolewa wafe kwa upanga, nao watakuwa chakula cha mbweha. Bali mfalme atafurahi katika Mungu, wale wote waapao kwa jina la Mungu watamsifu, bali vinywa vya waongo vitanyamazishwa.