Zaburi 63:1-11
Zaburi 63:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Ee Mungu, wewe u Mungu wangu, nami nakutafuta kwa moyo; roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu; nina kiu kama nchi kavu isiyo na maji. Nimetaka kukuona patakatifuni pako, niione nguvu yako na utukufu wako. Fadhili zako ni bora kuliko maisha, nami nitakusifu kwa mdomo wangu. Nitakushukuru maisha yangu yote; nitainua mikono yangu na kukuomba. Roho yangu inafurahi kama kwa karamu na vinono; kwa shangwe nitaimba sifa zako. Niwapo kitandani ninakukumbuka, usiku kucha ninakufikiria; maana wewe umenisaidia daima. Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia. Roho yangu inaambatana nawe kabisa, mkono wako wa kulia wanitegemeza. Lakini hao wanaotaka kuyaangamiza maisha yangu, watatumbukia chini kwenye makao ya wafu. Watauawa kwa upanga, watakuwa chakula cha mbweha. Lakini mfalme atafurahi kwa sababu ya Mungu; wanaoahidi kwa jina la Mungu watamsifu, lakini vinywa vya waongo vitafumbwa.
Zaburi 63:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee MUNGU, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, Mwili wangu wakuonea shauku, Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji. Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu, Nizione nguvu zako na utukufu wako. Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai; Midomo yangu itakusifu. Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai; Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu. Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono; Kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha. Ninapokukumbuka kitandani mwangu, Ninakutafakari usiku kucha. Maana Wewe umekuwa msaada wangu, Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia. Nafsi yangu inaambatana nawe sana; Mkono wako wa kulia unanitegemeza. Bali waitafutao nafsi yangu, ili kuiangamiza, Wataingia katika vilindi vya nchi. Watatolewa wafe kwa nguvu za upanga, Watakuwa riziki za mbwamwitu. Bali mfalme atamfurahia Mungu, Kila aapaye kwa Yeye atashangilia, Kwa maana vinywa vya waongo vitafumbwa.
Zaburi 63:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee MUNGU, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, Mwili wangu wakuonea shauku, Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji. Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu, Nizione nguvu zako na utukufu wako. Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai; Midomo yangu itakusifu. Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai; Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu. Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono; Kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha. Ninapokukumbuka kitandani mwangu, Nakutafakari Wewe makesha yote ya usiku. Maana Wewe umekuwa msaada wangu, Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia. Nafsi yangu inakuandama sana; Mkono wako wa kuume unanitegemeza. Bali waitafutao nafsi yangu, ili kuiharibu, Wataingia pande za nchi zilizo chini. Watatolewa wafe kwa nguvu za upanga, Watakuwa riziki za mbwa-mwitu. Bali mfalme atamfurahia Mungu, Kila aapaye kwa Yeye atashangilia, Kwa maana vinywa vya waongo vitafumbwa.
Zaburi 63:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu, nakutafuta kwa moyo wote; nafsi yangu inakuonea kiu, mwili wangu unakuonea wewe shauku, katika nchi kame na iliyochoka mahali ambapo hapana maji. Nimekuona katika mahali patakatifu na kuuona uwezo wako na utukufu wako. Kwa sababu upendo wako ni bora kuliko uhai, midomo yangu itakuadhimisha. Nitakusifu siku zote za maisha yangu, na kwa jina lako nitainua mikono yangu. Nafsi yangu itatoshelezwa kama kwa wingi wa vyakula; kwa midomo iimbayo kinywa changu kitakusifu wewe. Kitandani mwangu ninakukumbuka wewe, ninawaza juu yako makesha yote ya usiku. Kwa sababu wewe ndiwe msaada wangu, chini ya uvuli wa mbawa zako naimba. Nafsi yangu inaambatana nawe, mkono wako wa kuume hunishika. Wale wanaotafuta uhai wangu wataharibiwa, watakwenda chini kwenye vilindi vya dunia. Watatolewa wafe kwa upanga, nao watakuwa chakula cha mbweha. Bali mfalme atafurahi katika Mungu, wale wote waapao kwa jina la Mungu watamsifu, bali vinywa vya waongo vitanyamazishwa.