Zaburi 88
88
Zaburi 88
Kilio kwa ajili ya kuomba msaada
Wimbo. Zaburi ya wana wa Kora. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa mahalathi leanothi. Utenzi wa Hemani Mwezrahi.
1Ee Mwenyezi Mungu, Mungu uniokoaye,
nimelia mbele zako usiku na mchana.
2Maombi yangu yafike mbele zako,
utegee kilio changu sikio lako.
3Kwa maana nafsi yangu imejaa taabu,
na maisha yangu yanakaribia kaburi#88:3 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol..
4Nimehesabiwa miongoni mwa wale wanaoshuka shimoni;
niko kama mtu asiye na nguvu.
5Nimetengwa pamoja na wafu,
kama waliochinjwa walalao kaburini,
ambao huwakumbuki tena,
ambao wamekatiliwa mbali na uangalizi wako.
6Umenitupa katika shimo lenye kina kirefu sana,
katika vina vya giza nene.
7Ghadhabu yako imekuwa nzito juu yangu,
umenigharikisha kwa mawimbi yako yote.
8Umenitenga na rafiki zangu wa karibu
na kunifanya chukizo kwao.
Nimezuiliwa, wala siwezi kutoroka;
9nuru ya macho yangu
imefifia kwa ajili ya huzuni.
Ee Mwenyezi Mungu, ninakuita kila siku,
ninakunyooshea wewe mikono yangu.
10Je, wewe huwaonesha wafu maajabu yako?
Je, wale waliokufa huinuka na kukusifu?
11Je, upendo wako hutangazwa kaburini,
uaminifu wako katika Uharibifu#88:11 yaani Abadon?
12Je, maajabu yako hujulikana mahali pa giza,
au matendo yako ya haki katika nchi ya usahaulifu?
13Lakini ninakulilia wewe, Ee Mwenyezi Mungu, unisaidie;
asubuhi maombi yangu huja mbele zako.
14Ee Mwenyezi Mungu, kwa nini unanikataa
na kunificha uso wako?
15Tangu ujana wangu nimeteseka, nikakaribia kifo;
nimepatwa na mapigo yako, nami nimekata tamaa.
16Ghadhabu yako imepita juu yangu;
mapigo yako yameniangamiza.
17Mchana kutwa zinanizunguka kama mafuriko;
zimenimeza kabisa.
18Umeniondolea rafiki na wapendwa wangu;
giza limekuwa rafiki yangu wa karibu kuliko wote.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 88: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.