Zaburi 89
89
Zaburi 89
Wimbo wakati wa taabu ya kitaifa
Utenzi wa Ethani Mwezrahi.
1Nitaimba kuhusu upendo mkuu wa Mwenyezi Mungu milele;
kwa kinywa changu nitavijulisha
vizazi vyote uaminifu wako.
2Nitatangaza kuwa upendo wako unasimama imara milele
na uaminifu wako umeuthibitisha mbinguni.
3Ulisema, “Nimefanya agano na mteule wangu,
nimemwapia mtumishi wangu Daudi,
4‘Nitaimarisha uzao wako milele
na kudumisha ufalme wako kwa vizazi vyote.’ ”
5Ee Mwenyezi Mungu, mbingu zinayasifu maajabu yako,
uaminifu wako pia katika kusanyiko la watakatifu.
6Kwa kuwa ni nani katika mbingu
anayeweza kulinganishwa na Mwenyezi Mungu?
Ni nani miongoni mwa viumbe vya mbinguni
aliye kama Mwenyezi Mungu?
7Katika kusanyiko la watakatifu, Mungu huogopwa sana,
anahofiwa kuliko wote wanaomzunguka.
8Ee Bwana Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni,
ni nani aliye kama wewe?
Ee Mwenyezi Mungu, wewe ni mwenye nguvu,
na uaminifu wako unakuzunguka.
9Wewe unatawala bahari yenye msukosuko;
mawimbi yake yanapoinuka, wewe unayatuliza.
10Wewe ulimponda Rahabu#89:10 jina la Misri kwa fumbo
kama mmoja wa waliochinjwa;
kwa mkono wako wenye nguvu,
uliwatawanya adui zako.
11Mbingu ni zako, nayo nchi pia ni yako,
uliuwekea ulimwengu msingi
pamoja na vyote vilivyomo.
12Uliumba kaskazini na kusini;
Tabori na Hermoni wanaliimbia jina lako kwa furaha.
13Mkono wako umejaa uwezo;
mkono wako una nguvu,
mkono wako wa kuume umetukuka.
14Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako cha enzi;
upendo na uaminifu vinakutangulia.
15Heri ni wale ambao wamejifunza kukusifu kwa shangwe,
wanaotembea katika mwanga
wa uwepo wako, Ee Mwenyezi Mungu.
16Wanashangilia katika jina lako mchana kutwa,
wanafurahi katika haki yako.
17Kwa kuwa wewe ni utukufu na nguvu yao,
kwa wema wako unatukuza pembe#89:17 pembe inawakilisha nguvu yetu.
18Naam, ngao yetu ni mali ya Mwenyezi Mungu,
na mfalme wetu mali ya Aliye Mtakatifu wa Israeli.
19Ulizungumza wakati fulani katika maono,
kwa watu wako waaminifu, ukasema:
“Nimeweka nguvu kwa shujaa,
nimemwinua kijana miongoni mwa watu.
20Nimemwona Daudi, mtumishi wangu,
na nimempaka mafuta yangu matakatifu.
21Kitanga changu kitamtegemeza,
hakika mkono wangu utamtia nguvu.
22Hakuna adui atakayemtoza ushuru,
hakuna mtu mwovu atakayemtesa.
23Nitawaponda adui zake mbele zake
na kuwaangamiza watesi wake.
24Upendo wangu mkamilifu utakuwa pamoja naye,
kwa Jina langu pembe yake itatukuzwa.
25Nitauweka mkono wake juu ya bahari,
mkono wake wa kuume juu ya mito.
26Naye ataniita kwa sauti, ‘Wewe ni Baba yangu,
Mungu wangu, Mwamba na Mwokozi wangu.’
27Nitamteua pia awe mzaliwa wangu wa kwanza,
aliyetukuka kuliko wafalme wote wa dunia.
28Nitadumisha upendo wangu kwake milele,
na agano langu naye litakuwa imara.
29Nitaudumisha uzao wake milele,
kiti chake cha utawala kama mbingu zinavyodumu.
30“Kama wanawe wataacha amri yangu
na wasifuate sheria zangu,
31wakihalifu maagizo yangu
na kutoshika amri zangu,
32nitaadhibu dhambi yao kwa fimbo,
uovu wao kwa kuwapiga;
33lakini sitauondoa upendo wangu kwake,
wala sitausaliti uaminifu wangu kamwe.
34Mimi sitavunja agano langu
wala sitabadili lile ambalo midomo yangu imelitamka.
35Mara moja na kwa milele, nimeapa kwa utakatifu wangu,
nami sitamdanganya Daudi:
36kwamba uzao wake utaendelea milele,
na kiti chake cha enzi kitadumu mbele zangu kama jua;
37kitaimarishwa milele kama mwezi,
shahidi mwaminifu angani.”
38Lakini wewe umemkataa, umemdharau,
umemkasirikia sana mpakwa mafuta wako.
39Umelikana agano lako na mtumishi wako,
na umelinajisi taji lake mavumbini.
40Umebomoa kuta zake zote,
na ngome zake zote umezifanya kuwa magofu.
41Wote wapitao karibu wamemnyang’anya mali yake;
amekuwa dharau kwa majirani zake.
42Umeutukuza mkono wa kuume wa adui zake,
umewafanya watesi wake wote washangilie.
43Umegeuza makali ya upanga wake,
na hukumpa msaada katika vita.
44Umeikomesha fahari yake,
na kukiangusha kiti chake cha enzi.
45Umezifupisha siku za ujana wake,
umemfunika kwa vazi la aibu.
46Hata lini, Ee Mwenyezi Mungu? Utajificha milele?
Ghadhabu yako itawaka kama moto hata lini?
47Kumbuka jinsi maisha yangu yanavyopita haraka.
Ni kwa ubatili kiasi gani umemuumba mwanadamu!
48Ni mtu gani awezaye kuishi na asione kifo,
au kujiokoa mwenyewe kutoka nguvu za kaburi#89:48 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol.?
49Ee Bwana, uko wapi upendo wako mkuu wa mwanzoni,
ambao katika uaminifu wako ulimwapia Daudi?
50Bwana kumbuka jinsi mtumishi wako amesimangwa,
jinsi ninavyovumilia moyoni mwangu dhihaka za mataifa yote,
51dhihaka ambazo kwazo adui zako
wamenisimanga, Ee Mwenyezi Mungu,
ambazo kwazo wamesimanga
kila hatua ya mpakwa mafuta wako.
52Ahimidiwe Mwenyezi Mungu milele!
Amen na Amen.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 89: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.