Ufunuo 16:1-7
Ufunuo 16:1-7 NEN
Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mle Hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni, mkayamwage duniani hayo mabakuli saba ya ghadhabu ya Mungu.” Malaika wa kwanza akaenda akalimwaga hilo bakuli lake juu ya nchi. Majipu mabaya yenye maumivu makali yakawapata wale watu wote waliokuwa na chapa ya yule mnyama na walioabudu sanamu yake. Malaika wa pili akalimwaga bakuli lake baharini, nayo ikabadilika kuwa damu kama ya mtu aliyekufa na kila kiumbe hai kilichokuwa ndani ya bahari kikafa. Malaika wa tatu akalimwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, nazo zikawa damu. Ndipo nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema: “Wewe una haki katika hukumu hizi ulizotoa, wewe uliyeko, uliyekuwako, Uliye Mtakatifu, kwa sababu umehukumu hivyo; kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu wako na manabii wako, nawe umewapa damu wanywe kama walivyostahili.” Nikasikia madhabahu ikiitikia, “Naam, BWANA Mungu Mwenyezi, hukumu zako ni kweli na haki.”