Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 18:1-8

Ufunuo 18:1-8 NEN

Baada ya haya nikaona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni, akiwa na mamlaka makuu na dunia ikamulikiwa na mngʼao wake. Naye akalia kwa nguvu kwa sauti kubwa, akisema: “Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu! Umekuwa makao ya mashetani na makazi ya kila pepo mchafu, makazi ya kila ndege na kila mnyama achukizaye. Kwa maana mataifa yote yamekunywa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake. Nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi nao, nao wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na wingi wa utajiri wake.” Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema: “Tokeni katikati yake, enyi watu wangu, ili msije mkashiriki dhambi zake, ili msije mkapatwa na pigo lake lolote; kwa kuwa dhambi zake zimelundikana hadi mbinguni, naye Mungu ameukumbuka uhalifu wake. Mtendee kama yeye alivyotenda; umlipe mara mbili kwa ajili ya yale aliyotenda. Katika kikombe chake mchanganyie mara mbili ya kile alichochanganya. Mpatie mateso na huzuni nyingi sawa na utukufu na anasa alizojipatia. Kwa kuwa moyoni mwake hujivuna, akisema, ‘Mimi ninatawala kama malkia; mimi si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.’ Kwa hiyo mapigo yatampata kwa siku moja: mauti, maombolezo na njaa. Naye atateketezwa kwa moto, kwa maana BWANA Mungu amhukumuye ana nguvu.