Ufunuo 18
18
Kuanguka kwa Babeli
1Baada ya haya nikaona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni, akiwa na mamlaka kuu na dunia ikaangazwa kwa mng’ao wake. 2Naye akapaza sauti kwa nguvu, akisema:
“ ‘Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu!’#18:2 Isaya 21:9
Umekuwa makao ya mashetani
na makazi ya kila pepo mchafu,
makazi ya kila ndege na kila mnyama achukizaye.
3Kwa maana mataifa yote yamekunywa
mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.
Nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye,
na wafanyabiashara wa dunia
wametajirika kutokana na wingi wa utajiri wake.”
4Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema:
“ ‘Tokeni katikati yake, enyi watu wangu,’#18:4 Yeremia 51:45
ili msije mkashiriki dhambi zake,
ili msije mkapatwa na pigo lake lolote;
5kwa kuwa dhambi zake zimefika hadi mbinguni,
naye Mungu ameukumbuka uhalifu wake.
6Mtendee kama yeye alivyotenda;
umlipe mara mbili kwa ajili ya yale aliyotenda.
Katika kikombe chake mchanganyie
mara mbili ya kile alichochanganya.
7Mpatie mateso na huzuni nyingi sawa na
utukufu na anasa alizojipatia.
Kwa kuwa moyoni mwake hujivuna, akisema,
‘Mimi ninatawala kama malkia;
mimi si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.’#18:7 Isaya 47:7, 8
8Kwa hiyo mapigo yatampata kwa siku moja:
mauti, maombolezo na njaa.
Naye atateketezwa kwa moto,
kwa maana Mwenyezi Mungu amhukumuye ana nguvu.
9“Wafalme wa dunia waliozini naye na kushiriki anasa zake watakapoona moshi wa kuungua kwake, watamlilia na kumwombolezea. 10Kwa hofu kubwa ya mateso yake, watasimama mbali na kulia na wakisema:
“ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa,
ee Babeli mji wenye nguvu!
Hukumu yako imekuja katika saa moja!’
11“Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumwomboleza kwa sababu hakuna anunuaye bidhaa zao tena: 12Bidhaa za dhahabu, za fedha, za vito vya thamani na vya lulu, kitani safi, nguo za rangi ya zambarau, hariri, nguo nyekundu, aina zote za miti ya udi, na vifaa vyote vya pembe za ndovu, vifaa vyote vya miti yenye thamani kuliko yote, shaba, chuma na marumaru, 13bidhaa za mdalasini na vikolezo, za uvumba, manemane, na uvumba wenye harufu nzuri, za divai, na mafuta ya zeituni, za unga mzuri na ngano; ng’ombe na kondoo; farasi na magari ya vita; na miili na roho za wanadamu.
14“Watasema, ‘Yale matunda ambayo roho yako iliyatamani yamekoma. Utajiri wako wote na fahari yako vimetoweka, wala haviwezi kupatikana tena kamwe!’ 15Wale wafanyabiashara waliotajirika kwa bidhaa hizo kutoka kwake watasimama mbali naye kwa hofu kubwa ya mateso yanayompata. Watalia na kuomboleza, 16wakisema:
“ ‘Ole! Ole, ee mji mkuu,
uliyekuwa umevikwa mavazi ya kitani safi,
ya rangi ya zambarau na nyekundu,
ukimetameta kwa dhahabu,
vito vya thamani na lulu!
17Katika muda wa saa moja utajiri wote mkubwa
kama huu umeangamia!’
“Kila nahodha, na wote wasafirio kwa meli, na wote wapatao kipato chao kutokana na bahari, watasimama mbali. 18Watakapouona moshi wa kuungua kwake watalia wakisema, ‘Je, kulipata kuwako mji mkubwa kama huu?’ 19Nao watajirushia mavumbi vichwani mwao, huku wakilia na kuomboleza, wakisema:
“ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa,
mji ambao wote wenye meli baharini
walitajirika kupitia kwa mali yake!
Katika saa moja tu ameangamizwa!’
20“Furahia kwa ajili yake, ee mbingu!
Furahini watakatifu, mitume na manabii!
Mungu amemhukumu
kwa vile alivyowatendea ninyi.”
21Kisha malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe kubwa kama la kusagia, akalitupa baharini akisema:
“Hivyo ndivyo mji mkubwa Babeli
utakavyotupwa chini kwa nguvu,
wala hautaonekana tena.
22Nyimbo za wapiga vinubi na waimbaji,
wapiga filimbi na wapiga tarumbeta
kamwe hazitasikika tena ndani yako.
Ndani yako kamwe hataonekana tena fundi
mwenye ujuzi wa aina yoyote.
Wala sauti ya jiwe la kusagia
kamwe haitasikika tena.
23Mwanga wa taa
hautaangaza ndani yako tena.
Sauti ya bwana arusi na bibi arusi
kamwe haitasikika ndani yako tena.
Wafanyabiashara wako walikuwa watu maarufu wa dunia.
Mataifa yote yalipotoshwa kwa uchawi wako.
24Ndani yake ilionekana damu ya manabii na ya watakatifu,
na wote waliouawa duniani.”
Iliyochaguliwa sasa
Ufunuo 18: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.