Warumi 11:1-10
Warumi 11:1-10 NEN
Basi nauliza: Je, Mungu amewakataa watu wake? La, hasha! Mimi mwenyewe ni Mwisraeli, tena uzao wa Abrahamu kutoka kabila la Benyamini. Mungu hajawakataa watu wake, ambao yeye aliwajua tangu mwanzo. Je, hamjui yale Maandiko yasemayo kuhusu Eliya, jinsi alivyomlalamikia Mungu kuhusu Israeli? Alisema, “Bwana, wamewaua manabii wako na kuzibomoa madhabahu zako, nimebaki mimi peke yangu, nao wanataka kuniua?” Je, Mungu alimjibuje? “Nimejibakizia watu elfu saba ambao hawajapiga magoti kumwabudu Baali.” Vivyo hivyo pia, sasa wapo mabaki waliochaguliwa kwa neema ya Mungu. Lakini ikiwa wamechaguliwa kwa neema, si tena kwa msingi wa matendo. Kama ingekuwa kwa matendo, neema isingekuwa neema tena. Tuseme nini basi? Kile kitu ambacho Israeli alikitafuta kwa bidii hakukipata. Lakini waliochaguliwa walikipata. Waliobaki walifanywa wagumu, kama ilivyoandikwa: “Mungu aliwapa bumbuazi la mioyo, macho ili wasiweze kuona, na masikio ili wasiweze kusikia, hadi leo.” Naye Daudi anasema: “Karamu zao na ziwe tanzi na mtego wa kuwanasa, kitu cha kuwakwaza waanguke, na adhabu kwao. Macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona, nayo migongo yao iinamishwe daima.”