Rum 11:1-10
Rum 11:1-10 SUV
Basi, nauliza, Je! Mungu aliwasukumia mbali watu wake? Hasha! Kwa kuwa mimi nami ni Mwisraeli, mmoja wa wazao wa Ibrahimu, mtu wa kabila ya Benyamini. Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu, Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu. Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali. Basi ni vivi hivi wakati huu wa sasa, yako mabaki waliochaguliwa kwa neema. Lakini ikiwa ni kwa neema, haiwi kwa matendo tena, au hapo neema isingekuwa neema. Imekuwaje basi? Kitu kile ambacho Israeli alikuwa akikitafuta hakukipata; lakini wale waliochaguliwa walikipata, na wengine walitiwa uzito. Kama ilivyoandikwa, Mungu aliwapa roho ya usingizi, macho hata wasione, na masikio hata wasisikie, hata siku hii ya leo. Na Daudi asema, Meza yao na iwe tanzi na mtego, Na kitu cha kuwakwaza, na malipo kwao; Macho yao yatiwe giza ili wasione, Ukawainamishe mgongo wao siku zote.