Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Warumi 11

11
Mabaki ya Israeli
1Basi nauliza: Je, Mungu amewakataa watu wake? La, hasha! Mimi mwenyewe ni Mwisraeli, tena uzao wa Ibrahimu kutoka kabila la Benyamini. 2Mungu hajawakataa watu wake, ambao yeye aliwajua tangu mwanzo. Je, hamjui yale Maandiko yasemayo kuhusu Ilya, jinsi alivyomlalamikia Mungu kuhusu Israeli? 3Alisema, “Mwenyezi Mungu, wamewaua manabii wako na kuzibomoa madhabahu zako, nimebaki mimi peke yangu, nao wanataka kuniua?”#11:3 1 Wafalme 19:10, 14 4Je, Mungu alimjibuje? “Nimejibakizia watu elfu saba ambao hawajapiga magoti kumwabudu Baali.”#11:4 1 Wafalme 19:18 5Vivyo hivyo pia, sasa wapo mabaki waliochaguliwa kwa neema ya Mungu. 6Lakini ikiwa wamechaguliwa kwa neema, si tena kwa msingi wa matendo. Kama ingekuwa kwa matendo, neema isingekuwa neema tena.
7Tuseme nini basi? Kile kitu ambacho Israeli alikitafuta kwa bidii hakukipata. Lakini waliochaguliwa walikipata. Waliobaki walifanywa wagumu, 8kama ilivyoandikwa:
“Mungu aliwapa bumbuazi la mioyo,
macho ili wasiweze kuona,
na masikio ili wasiweze kusikia,
hadi leo.”#11:8 Kumbukumbu 29:4; Isaya 29:10
9Naye Daudi anasema:
“Karamu zao na ziwe tanzi na mtego wa kuwanasa,
kitu cha kuwakwaza waanguke, na adhabu kwao.
10Macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona,
nayo migongo yao iinamishwe daima.”#11:10 Zaburi 69:22, 23
Matawi yaliyopandikizwa
11Hivyo nauliza tena: Je, Waisraeli walijikwaa ili waanguke na kuangamia kabisa? La, hasha! Lakini kwa sababu ya makosa yao, wokovu umewafikia watu wa Mataifa, ili kuwafanya Waisraeli waone wivu. 12Basi ikiwa kukosa kwao kumekuwa utajiri mkubwa kwa ulimwengu, tena kama kuangamia kwao kumeleta utajiri kwa watu wa Mataifa, kurudishwa kwao kutaleta utajiri mkuu zaidi.
13Sasa ninasema nanyi watu wa Mataifa. Maadamu mimi ni mtume kwa watu wa Mataifa, naitukuza huduma yangu 14ili kuwafanya watu wangu waone wivu na hivyo kuwaokoa baadhi yao. 15Kwa kuwa ikiwa kukataliwa kwao ni kupatanishwa kwa ulimwengu, kukubaliwa kwao si kutakuwa ni uhai baada ya kufa? 16Kama sehemu ya donge la unga uliotolewa kuwa limbuko ni mtakatifu, basi unga wote ni mtakatifu, nalo shina kama ni takatifu, vivyo hivyo na matawi nayo.
17Lakini kama baadhi ya matawi yalikatwa, nawe chipukizi la mzeituni mwitu ukapandikizwa mahali pao ili kushiriki unono pamoja na matawi mengine kutoka shina la mzeituni, 18basi usijivune juu ya hayo matawi. Lakini ukijivuna, kumbuka jambo hili: Si wewe unayelishikilia shina, bali ni shina linalokushikilia wewe. 19Basi utasema, “Matawi yale yalikatwa ili nipate kupandikizwa katika hilo shina.” 20Hii ni kweli. Matawi hayo yalikatwa kwa sababu ya kutokuamini kwake, lakini wewe umesimama tu kwa sababu ya imani. Kwa hiyo usijivune, bali simama kwa kuogopa. 21Kwa maana kama Mungu hakuyahurumia matawi ya asili, wala hatakuhurumia wewe.
22Angalia basi wema na ukali wa Mungu: Ukali kwa wale walioanguka, bali wema wa Mungu kwako wewe, kama utadumu katika wema wake. La sivyo, nawe utakatiliwa mbali. 23Wao nao wasipodumu katika kutokuamini kwao, watapandikizwa tena kwenye shina, kwa maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena kwenye hilo shina. 24Ikiwa wewe ulikatwa kutoka kile ambacho kwa asili ni mzeituni mwitu, na kupandikizwa kinyume cha asili kwenye mzeituni uliopandwa, si rahisi zaidi matawi haya ya asili kupandikizwa tena kwenye shina lake la mzeituni wao mwenyewe!
Israeli wote wataokolewa
25Ndugu zangu, ili msije mkajidai kuwa wenye hekima kuliko mlivyo, nataka mfahamu siri hii: Ugumu umewapata Israeli kwa sehemu hadi idadi ya watu wa Mataifa watakaoingia itimie. 26Hivyo Israeli wote wataokolewa. Kama ilivyoandikwa:
“Mkombozi atakuja kutoka Sayuni;
ataondoa kutokumcha Mungu katika Yakobo.
27Hili ndilo agano langu nao
nitakapoziondoa dhambi zao.”#11:27 Isaya 59:20, 21; 27:9; Yeremia 31:33, 34
28Kwa habari ya Injili, wao ni adui wa Mungu kwa ajili yenu, lakini kuhusu kule kuteuliwa kwao ni wapendwa, kwa ajili ya baba zao wa zamani; 29kwa maana akishawapa watu karama, Mungu haziondoi, wala wito wake. 30Kama vile ninyi wakati fulani mlivyokuwa waasi kwa Mungu lakini sasa mmepata rehema kwa sababu ya kutokutii kwao, 31hivyo nao Waisraeli wamekuwa waasi ili wao nao sasa waweze kupata rehema kwa ajili ya rehema za Mungu kwenu. 32Kwa maana Mungu amewafunga wanadamu wote kwenye kuasi ili apate kuwarehemu wote.
Wimbo wa shukrani
33Tazama jinsi kilivyo kina cha utajiri
wa hekima na maarifa ya Mungu!
Tazama jinsi hukumu zake hazichunguziki,
na ambavyo njia zake hazitafutiki!
34“Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Mwenyezi Mungu?
Au ni nani ambaye amekuwa mshauri wake?”#11:34 Isaya 40:13
35“Au ni nani aliyempa chochote
ili arudishiwe?”#11:35 Ayubu 41:11
36Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake,
viko kwake na kwa ajili yake.
Utukufu ni wake milele! Amen.

Iliyochaguliwa sasa

Warumi 11: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia