Warumi 10
10
1Ndugu zangu, shauku ya moyo wangu na maombi yangu kwa Mungu ni kwa ajili ya Waisraeli, kwamba waokolewe. 2Kwa maana ninaweza nikashuhudia wazi kwamba wao wana juhudi kubwa kwa ajili ya Mungu, lakini juhudi yao haina maarifa. 3Kwa kuwa hawakuijua haki ya Mungu, wakatafuta kuweka haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu. 4Kwa maana Al-Masihi ni ukomo wa sheria ili kila mtu aaminiye ahesabiwe haki.
Wokovu kwa watu wote
5Musa anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.”#10:5 Walawi 18:5 6Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’#10:6 Kumbukumbu 30:12” (yaani ili kumleta Al-Masihi chini) 7“au ‘Ni nani atashuka kwenda Kuzimu#10:7 Kuzimu hapa kwa Kiyunani ni Abyss, yaani mahali pa wafu.?’#10:7 Kumbukumbu 30:13” (yaani ili kumleta Al-Masihi kutoka kwa wafu). 8Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,”#10:8 Kumbukumbu 30:14 yaani lile neno la imani tunalolihubiri. 9Kwa sababu, ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Isa ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. 10Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu. 11Kama Maandiko yanavyosema, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.”#10:11 Isaya 28:16 12Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na mtu wa Mataifa, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. 13Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Mwenyezi Mungu, ataokolewa.”#10:13 Yoeli 2:32
14Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? 15Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri Habari Njema!”#10:15 Isaya 52:7
16Lakini si wote waliotii Injili. Kwa maana Isaya asema, “Mwenyezi Mungu, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?”#10:16 Isaya 53:1 17Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Al-Masihi. 18Lakini nauliza: Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, kwa maana:
“Sauti yao imeenea duniani pote,
nayo maneno yao yameenea
hadi miisho ya ulimwengu.”#10:18 Zaburi 19:4
19Nami nauliza tena: Je, Waisraeli hawakuelewa? Kwanza, Musa asema,
“Nitawafanya mwe na wivu
kwa watu wale ambao si taifa.
Nitawakasirisha kwa taifa
lile lisilo na ufahamu.”#10:19 Kumbukumbu 32:21
20Naye Isaya kwa ujasiri mwingi anasema,
“Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta.
Nilijifunua kwa watu
wale ambao hawakunitafuta.”#10:20 Isaya 65:1
21Lakini kuhusu Israeli anasema,
“Mchana kutwa nimewanyooshea
watu wakaidi na wasiotii mikono yangu.”#10:21 Isaya 65:2
Iliyochaguliwa sasa
Warumi 10: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.